• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
KINYANG’ANYIRO 2022: Pokot Magharibi

KINYANG’ANYIRO 2022: Pokot Magharibi

UKUBWA: kilomita mraba 9,169

IDADI YA WATU: 621, 241

WAPIGAKURA: 220,026

MAENEO BUNGE: Kapenguria, Kacheliba, Pokot Kusini na Sigor

NA OSCAR KAKAI

Pokot Magharibi ni kaunti nambari 024 na ni kati ya kaunti 14 zinazopatikana kwenye bonde la ufa, ambalo zamani lilijulikana kama Mkoa wa Rift Valley.

Inapakana na nchi jirani ya Uganda upande wa Magharibi, Kaunti jirani za Baringo na Elgeyo Marakwet pande za Mashariki na Kusini Mashariki mtawalia. Trans Nzoia iko Kusini na kaunti kubwa zaidi nchini (Turkana) inapakana nayo pande na Kaskazini na Kaskazini Mashariki.

Ingawa kuna mseto wa jamii mbalimbali, asilimia kubwa ya watu walio kwenye kaunti hii ni jamii ya Wapokot, ambalo ni kabila dogo la Wakalenjin.

Ingawa kuna miji mingine kama vile Sigor, Kongelai na Chepareria, makao makuu yako mjini Kapenguria. Ni mji huu ulio na historia muhimu ya taifa la Kenya, ambako Mzee Jomo Kenyatta na wenzake watano walifungwa jela na serikali ya mkoloni mwaka 1952, walipokuwa wakipigania uhuru wa Kenya. Wenzake walikuwa Achieng’ Oneko, Kung’u Karumba, Paul Ngei, Bildad Kagia na Fred Kubai.

Pokot Magharibi ina mbuga za wanyama za Kapenguria, Mlima Mtello, Nasalot na mabwawa ya kuvutia ya Turkwel, Tartar na Gorge.

Mlima Elgon unapatikana ndani ya kaunti hii na ndiko uliko mradi mkubwa wa kawi ya mvuke wa Turkwell.

Mwanariadha maarufu Tegla Lorupe ni kati ya watu mashuhuri kutoka Pokot Magharibi.

UGAVANA

PROF JOHN LONYANGAPUO (KUP)

Alizaliwa 1954 Anatetea wadhifa huo kupitia chama alichounda cha Kenya Union Party.

Alichukua wadhifa huo 2017 alipomshinda Simon Kachapin.? Ni mwalimu na amewahi kuhudumu kama seneta wa kaunti hiyo kati ya 2013-2017.

MANIFESTO: Kuhakikisha usawa, kuboresha uchumi na kuimarisha viwango vya elimu. Pia ameahidi kutoa mazingira bora ya uwekezaji, kuboresha miundomsingi na pia kutoa nafasi ya ajira ili vijana wajitegemee kimapato.

Uwekezaji, Uzalishaji wa mapato, Miundomsingi, Elimu, Afya, Kilimo, Ufugaji, Maji, Utalii, Michezo na Ukuzaji Talanta, Amani na Usalama.

SIMON KACHAPIN (UDA)

Alizaliwa 1967 Ana digrii ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Moi na alikuwa Mwalimu. Ndiye aliyechaguliwa gavana wa kwanza 2003. Kabla ya kujiuzulu Februari, alikuwa waziri msaidizi (CAS) wa Michezo na Utamaduni na pia akashikilia Kawi.

MANIFESTO: Analenga kupambana na ufisadi, kuimarisha uchumi wa eneo hilo na kuimarisha huduma za afya na pia elimu.

DKT NICHOLAS ATUDONYANG’

Alizaliwa 1981 Ana digrii ya Udaktari na Upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Amehudumu kama Naibu Gavana kwa Prof Lonyangapuo. Ingawa amekuwa nje ya nchi kwa muda mrefu, analenga kuchukua wadhifa huo kutoka kwa bosi wake.

MANIFESTO: Kupambana na ufisadi, kuboresha elimu na kushiriki miradi ya kuinua jamii.

WAWANIAJI WA KITI CHA MWAKILISHI WA KIKE

LILLIAN TOMITOM (UDA)

Ndiye mbunge wa sasa aliyechaguliwa 2017 kupitia chama cha Jubilee.

Ana digrii ya Elimu (Kiingereza na Fasihi) kutoka Chuo Kikuu cha Moi. Pia ana shahada ya uzamili katika Usimamizi wa Wafanyikazi, Moi University.

Mwaniaji kiti cha Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Pokot Magharibi Lillian Tomitom kwa tikiti ya UDA. PICHA | MAKTABA

Kabla ya kuingia siasa, alikuwa Mwalimu shule ya upili ya Chesta Girls na akawa msimamizi katika vyuo vikuu vya Eldoret na Moi.

Kati ya malengo yake ni kuimarisha masomo ya mtoto wa kike, pamoja na kuwainua vijana na akina mama kwa kubuni nafasi za ajira.

RAEL CHEPKEMOI KASWAI (KUP)

Ni mwalimu kitaaluma.

Kabla ya kujitosa kwenye siasa, alikuwa mwalimu mkuu. Amewarai wakazi wamchague akiahidi kupigania maslahi ya watu wanaoishi na ulemavu pamoja na kuwainua kimapato vijana na akina mama mashinani.

HELEN CHEROTICH (CCM)

Chama anachotumia kinaongozwa na gavana wa zamani wa Bomet Isaac Ruto.

Taifa Leo haikufanikiwa kumfikia ili kuelewa manifesto yake kati ya masuala mengine kwenye kampeni yake.

NIGHT CHEROP CHONGORIO (HURU)

Yeye ni mfanyabiashara.

Analenga kuimarisha masomo ya mtoto wa kike na pia kupambana na ukeketaji pamoja na ndoa za mapema.

CATHERINE CHEPKEMOI MUKENYANG (KANU)

Amehudumu kama Spika wa Bunge la Pokot Magharibi.

Katika mikutano yake ya kampeni anasema pia atapigania maslahi ya akina mama, kuwainua kibiashara na pia kuimarisha sekta ya afya ili kuimarisha huduma kwa akina mama wanaojifungua.

RODAH CHEPKOPUS ROTINO (ODM)

Alikuwa Waziri wa Michezo na Utamaduni katika Kaunti ya Pokot Magharibi. Anatarajia kuyashughulikia maslahi ya wakongwe na pia kuimarisha elimu kwa mtoto wa kike.

USENETA

Samuel Poghisio – Kanu

Bw Poghisio ni seneta wa sasa na anatetea wadhifa wake kupitia Kanu inayoongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi

Geoffrey Lipale – KUP

Julius Murgor – UDA

Dennis Ruto Kapchok (Mulmulwas) – Safina

WAWANIAJI UBUNGE

KAPENGURIA

Samuel Moroto – UDA

Philemon Lutodo – KUP

Philomena Chenangat-Jubilee

Haron Rumaita – Kanu

Nicholas Siwatom

SIGOR

Peter Lochakapong – UDA

Philip Rotino -KUP

Julius Ariwomoi – KANU

KACHELIBA

Mark Lomunokol ( mbunge wa sasa)– UDA

Titus Lotee- KUP

John Lodinyo –Kanu

POKOT KUSINI

Simon Kalekem – UDA

David Pkosing – KUP

James Tekoo-Mwaniaji huru

  • Tags

You can share this post!

Miriam Osimbo: Nimejiwekea malengo ya kumiliki brandi ya...

Wajackoyah ampa Raila bonga points

T L