• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:15 PM
Wajackoyah ampa Raila bonga points

Wajackoyah ampa Raila bonga points

BENSON MATHEKA Na RUSHDIE OUDIA

MGOMBEA urais wa chama cha Roots Party, George Wajackoyah amewasisimua wafuasi wa mgombea urais wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kufuatia kauli alizotoa kwenye kampeni zake Kisumu zilizoashiria anaweza kuwa mradi wake.

Akiwa katika kampeni mjini Kisumu mnamo Jumatatu, Prof Wajackoyah alitoa matamshi yaliyoonyesha kuwa huenda ana mkataba wa ushirikiano na Bw Odinga au amedhaminiwa na kiongozi huyo wa ODM kutimiza maslahi yake katika uchaguzi mkuu ujao.

Msomi huyo mwanasiasa alianza kwa kuelezea historia yake na familia ya Bw Odinga, akisema alikuwa akionha mlo wa babake Bw Odinga, marehemu Jaramogi Oginga Odinga kabla hajala.

Alisema kwamba iwapo atashinda urais, ataketi na Bw Odinga wapange jinsi ya kuongoza nchi, akiongeza kuwa ushindi wake au wa Bw Odinga ni ushindi wa eneo la magharibi mwa Kenya. Bw Wajackoyah anatoka Kaunti ya Kakamega ilhali Bw Odinga anatoka Siaya.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika mtaa wa Kondele jijini Kisumu, Prof Wajackoyah alisema kwamba alitumwa na Bw Odinga kumwandalia njia kuelekea ikulu.

“Mimi nasema hivi, kwa sababu Agwambo amenituma akaniambia mwana wa Omwami, wewe tangulia, tembea huko na ukifika hapo simama. Nikisimama nitakuwa na kitu cha kufanya huku Raila akiwa Ikulu akinipatia maagizo,” Prof Wajackoyah alisema kwa lugha ya Kijaluo.

Wakazi walichukulia kauli yake kumaanisha kuwa ana makubaliano ya siri na Bw Odinga kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, huku wadadisi wakisema huenda anatumiwa kuvutia kura za vijana ambao wamekuwa wakishabikia sera zake.

BANGI

Bw Wajackoyah ameahidi kuwa atahalalisha ukuzaji wa bangi nchini kwa ajili ya mauzo ng’ambo na kutumia pesa zitakazopatikana kulipa madeni ya taifa na kuinua maisha ya Wakenya. Ahadi zingine zake ni kuimarisha ufugaji wa nyoka kwa ajili ya sumu yake, kuwaua watu wafisadi na kupunguza siku rasmi za kazi kutoka tano hadi nne kwa wiki.

“Hata Agwambo amekubali na ameniambia kwamba watu hawa wamemhujumu, wameiba kura zake na hata kumtupa gerezani na ndio sababu aliniweka na kunisukuma polepole, na utafikia wakati atajitokeza kuwa ndiye kigogo,” alisema Bw Wajackoyah.

Kauli zake ziliwakanganya wafuasi wa Bw Odinga.

“Huyu Wajackoyah nadhani ni mradi wa Raila. Nilivyomsikia akisifu Raila kila mahali na kupinga Ruto, ananishangaza,” mwanabodaboda mmoja jijini Kisumu alishangaa.

Katika mikutano yake ya kampeni Kaunti ya Kisumu ambayo ni ngome ya Bw Odinga, Prof Wajackoyah hakumshambulia.

“Nimekuja nyumbani kwa Baba na nilipokuwa nikija hapa, niliambiwa nikifika Kisumu, nisithubutu kumtusi Raila kwa sababu nitaona moto. Kuna huyo kijana kutoka Sugoi ambaye huwa anamtusi Raila akija hapa. Mwambieni aachane na Baba,” alisema.

Katika kampeni yake Kisumu, aliwapigia debe wagombeaji wa ODM wa viti vya ubunge kama Babu Owino (Embakasi Mashariki), Phelix Odiwuor, anayefahamika kama Jalangó (Lang’ata) na mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, aliyemtaja kama kaka yake.

Bw Odinga na washirika wake wa karibu hawajakosoa hadharani mapendekezo ya Prof Wajackoyah hasa kuhusu uhalalishaji wa bangi na hata kama wamefanya hivyo, hawajajitokeza wazi.

Siku tatu kabla ya kuzuru Kaunti ya Kisumu, dada mdogo wa Bw Odinga, Ruth Odinga, anayegombea kiti cha mwakilishi wa kike kaunti ya Kisumu alichapisha picha katika mitandao ya kijamii akiwa na Prof Wajackoyah.

Katika maelezo kuhusu picha hiyo, Bi Odinga alimtaja mgombeaji urais huyo kama kaka yake na kumwalika ajiunge na Azimio.

  • Tags

You can share this post!

KINYANG’ANYIRO 2022: Pokot Magharibi

Familia ya Cohen kutoa ushahidi zaidi

T L