• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:50 AM
Kufeli sekondari hakukumzuia kuwa Rais

Kufeli sekondari hakukumzuia kuwa Rais

Na MARY WANGARI

Bi Samia Suluhu, 61, aliyeapishwa Ijumaa kama rais wa sita wa Tanzania, ni mwanamke aliyeandikisha historia mara kadha, tangu alipojibwaga kwenye ulingo wa siasa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Mama huyu wa watoto wanne, alipanda ngazi ghafla kutoka wadhifa wa makamu wa rais na kutawazwa kama rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na kanda ya Afrika Mashariki.

Bi Suluhu ambaye pia alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa naibu rais wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki, alijipata katika afisi hiyo kuu zaidi baada ya kifo cha ghafla cha Rais John Pombe Magufuli kilichotangazwa Jumatano.

Rais Suluhu, aliyekuwa mfuasi sugu wa Bw Magufuli, na anayefahamika kwa upole na maneno machache, ni mwanamke wa Kiislamu aliyejitosa siasani mnamo 2000.

Alizaliwa Januari, 27, 1960 katika Kisiwa cha Zanzibar kilichokuwa kituo kikuu cha biashara ya watumwa na ambacho wakati huo hakikuwa kimeungana na Tanzania hadi miaka minne baadaye 1964.

Babake alikuwa mwalimu huku mamake akiwa mke nyumbani. Bi Suluhu ambaye amewahi kutangaza hadharani kuhusu matokeo yake duni shuleni, alikamilisha masomo yake ya sekondari mnamo 1977.

Alipata kazi kama karani katika afisi ya serikali akiwa na umri wa miaka 17.

Alifunga ndoa mwaka mmoja baadaye mnamo 1978 na mume wake Bw Hafidh Ameir, ambaye ni afisa wa kilimo aliyestaafu na ambaye pamoja wamejaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na msichana mmoja.

Wakati wote huo, alikuwa akifanya kozi fupifupi na hatimaye akafuzu kwa cheti cha Stashahada katika Taaluma ya Usimamizi wa Umma kutoka Chuo Kikuu cha Nzumbe.

Juhudi zake zilizaa matunda alipopandishwa cheo kama afisa wa maendeleo katika serikali ya Zanzibar mnamo 1988.

Baadaye, alipata kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula (WFP) na miaka miwili baadaye mnamo 1990, akateuliwa mkurugezi wa shirika kuu lisilo la kiserikali Zanzibar.

Akiwa hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kusomea Stashahada ya Uchumi na kufuzu mnamo 1994.

Alijitosa kwenye ulingo wa siasa kwa mara ya kwanza mnamo 2000, alipoteuliwa kama waziri katika Bunge la Zanzibar, na aliyekuwa Rais wakati huo, Abeid Amani Karume.

Alihudumu kama waziri wa ajira kwa vijana, waziri anayesimamia masuala ya wanawake na watoto, waziri wa utalii na uwekezaji wa biashara mtawalia katika Kisiwa cha Zanzibar.

You can share this post!

Chama cha Ruto chaaibishwa uchaguzini Machakos

TZ YAPATA SULUHU BAADA YA POMBE