• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Kwa Gachagua ‘mambo imechemka’ akipigwa vijembe kuwa ameshuka bei

Kwa Gachagua ‘mambo imechemka’ akipigwa vijembe kuwa ameshuka bei

NA LABAAN SHABAAN

KAULI ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba anataka kuingia katika handisheki na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta imeendelea kuibua gumzo kote nchini.

Bw Gachagua aliwarai viongozi wa Mlima Kenya wawe na umoja kwenye mahojiano aliyofanyiwa na kituo cha redio kinachopeperusha matangazo kwa lugha ya Gikuyu cha Inooro FM mnamo Ijumaa, Oktoba 6, 2023.

Naibu Rais alisema wamekubaliana na viongozi wote wa kisiasa katika ukanda huo kukoma kumshambulia Bw Kenyatta na badala yake wamheshimu.

“Ninapanga kufanya mazungumzo na Uhuru Kenyatta. Nimemwagiza kila mmoja kumheshimu, na anafanya vizuri kuendelea kufurahia amani yake,” akasema Bw Gachagua ambaye amekuwa akimshambulia rais mstaafu kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Mwenyekiti wa Baraza la Kumshauri Rais William Ruto kuhusu maswala ya Kiuchumi Dkt David Ndii, ameweka chapisho kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), akionekana kumchamba Bw Gachagua kwa vijembe.

Hivi punde zaidi, Bw Ndii ameonekana kumkejeli Bw Gachagua kuwa ameshuka bei na kurudi katika hali yake ya awali ya kuwa msaidizi wa Bw Kenyatta na kiongozi wa eneo wala si taifa.

“Hali yake ya msingi ni Mwenyekiti wa Muungano wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Wanaoishi Nyeri (NDUSA), Mkuu Maalum wa Tarafa ya Oyugis, Msaidizi wa Uhuru na kadhalika,” akasema Dkt Ndii katika mtandao wa kijamii wa X.

Dkt Ndii alikuwa akitoa maoni yake baada ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kulinda Watumiaji Bidhaa nchini Kenya (COFEK) Stephen Mutoro kumkashifu Naibu Rais.

Bw Mutoro amemshutumu Bw Gachagua kwa kile anachosema ni kutoa matamshi ovyo ovyo.

Harakati za Naibu Rais za kuonekana na kujisawiri ni mtetezi wa masilahi ya eneo la Mlima Kenya zimeibua hisia tofauti miongoni mwa viongozi wa kisiasa ndani ya serikali na katika upinzani.

Rais William Ruto akihutubu akiwa Kaunti ya Siaya mnamo Ijumaa, alipinga msimamo wa mdogo wake akisisitiza kuwa kila eneo lina mgao katika serikali ya Kenya Kwanza, bila kujali ikiwa lilimpigia kura au la.

Rais Ruto alitaja kauli ya “wenye hisa katika serikali” kuwa ya kipuuzi na iliyopitwa na wakati.

  • Tags

You can share this post!

Katuni Oktoba 7, 2023

Wapangaji wajionea sinema ya bure landilodi akidaiwa na...

T L