• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maandamano ya Azimio sasa kufanyika kila Jumatatu na Alhamisi

Maandamano ya Azimio sasa kufanyika kila Jumatatu na Alhamisi

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI  wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga sasa ametangaza kuwa maandamano yatakuwa yakifanyika jijini Nairobi na maeneo mengine nchini Jumatatu na Alhamisi kila wiki kuishinikiza serikali kutekeleza matakwa yake.

Haya ni pamoja na kupunguzwa gharama ya maisha, kufunguliwa kwa ‘server’ ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kushirikishwa kwa upinzani katika mchakato wa uteuzi wa mwenyekiti wa tume hiyo na makamishna sita.

Kwenye kikao na wanahabari kupitia runinga ya Azimio TV, Jumanne, Machi 21, 2023, Bw Odinga pia amesema kuanzia sasa wafuasi wa Azimio watasusia huduma na bidhaa za kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, Benki ya Kenya Commercial (KCB) na Shirika la Habari la Radio Africa, haswa magazeti ya The Star.

“Hii ni kwa sababu tumegundua kuwa kampuni hizi zinaendeleza dhuluma ambazo zinaendelezwa na serikali dhalimu ya William Ruto,” akasema Bw Odinga.

Mnamo Jumatatu, Bw Odinga alikuwa ametangaza kuwa Azimio itakuwa ikifanya maandamano kila Jumatatu kila wiki.

Vile vile, Bw Odinga alilaumu mkuu wa polisi Adamson Bungei kwa kuamuru maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kisiasa dhidi ya waandamanaji wa Azimio “ambao walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba.”

“Tutawasilisha kesi mahakamani humu nchini na katika ngazi za kimataifa hadi wakati ambapo tutapata haki,” akasema Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

KNCHR yaanza uchunguzi kuhusu uvunjaji wa haki za binadamu...

Viongozi wa UDA wataka Raila akamatwe, atiwe hatiani

T L