• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Magavana wa eneo la Gusii waonekana kuzima moto wa migogoro na manaibu wao

Magavana wa eneo la Gusii waonekana kuzima moto wa migogoro na manaibu wao

NA WYCLIFFE NYABERI

BAADA ya kukwaruzana na kulaumiana kwa muda, hatimaye magavana kutoka eneo la Gusii wameonekana kuzizika tofauti zao za kisiasa na manaibu wao.

Sasa naibu magavana hao wanahudhuria hafla za umma pamoja na wakubwa wao, kinyume na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakizisusia.

Naibu Gavana wa Nyamira Dkt James Gesami ndiye aliyekuwa wa kwanza kutofautiana na mkubwa wake ambaye ni Gavana Amos Nyaribo pindi tu waliposhinda uchaguzi wa Agosti 9, 2022, kupitia chama cha United Progressive Alliance (UPA).

Gavana Nyaribo alipolitaja Baraza lake la Mawaziri, Dkt Gesami alijitokeza na kusema hakuhusishwa kikamilifu katika uundwaji wa baraza hilo lakini Bw Nyaribo alikana madai hayo.

Kufuatia malumbano kati ya wawili hao, Dkt Gesami ‘alipotea’ na hakuwa akionekana katika shughuli nyingi za serikali ya Kaunti ya Nyamira zilizokuwa zikiongozwa na mkubwa wake.

Kulipotokea hoja iliyolenga kumng’atua mamlakani Bw Nyaribo mwezi Oktoba lakini ikaanguka, gavana akiwahutubia wanahabari alidai kuwa naibu wake alihusika kwa njia moja au nyingine katika upangaji wa hoja hiyo.

Dkt Gesami hata hivyo alikanusha madai hayo baadaye na kusema hakuwa na mipango wala nia yoyote fiche.

Lakini hivi karibuni, Dkt Gesami na Bw Nyaribo wameonekana pamoja, ishara kwamba huenda wameimarisha uhusiano wao.

Mnamo Desemba 10, 2023, wawili hao walihudhuria hafla ya kuchangisha pesa katika Kanisa Katoliki la Kenyambi.

Nayo Desemba 16, 2023, viongozi hao wa Nyamira walishiriki pamoja mchango mwingine wa kuchangisha pesa katika kaunti jirani ya Kisii. Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walikuwa wageni wakuu.

Kwa takribani mwezi mmoja uliopita katika Kaunti ya Kisii, uhusiano wa Dkt Robert Monda na Gavana Simba Arati ulionekana kuingia doa pale Dkt Monda aliwakaribisha nyumbani kwake wakosoaji wa gavana Arati.

Hatua hiyo haikuchukuliwa vyema miongoni mwa wandani wa gavana na Dkt Monda waliomkashifu kwa kila aina.

Lakini wiki jana, Dkt Monda alijiunga na gavana Arati katika hafla moja ya kaunti na kusema hakuwa akipanga njama yoyote na mahasimu wa kisiasa wa mkubwa wake.

Dkt Monda alikariri kwamba bado anazidi kumuunga mkono Bw Arati kwani wana wajibu kikatiba kuwatumikia wenyeji na wakazi wa Kisii.

“Mimi niko nyuma ya gavana Arati mia fil mia. Nitazidi kumuunga mkono na hatua yangu ya kukutana na wakosoaji wa gavana haifai kusawiriwa kama usaliti,” Dkt Monda akasema.

Alipohudhuriia hafla ya kuchangisha pesa katika eneo la Mosocho Jumamosi iliyopita, Rais Ruto aliwataka viongozi wote waliochaguliwa kutoka eneo pana la Gusii kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili wawahudumie raia.

  • Tags

You can share this post!

Ruto akiri kuongoza nchi kama Rais si mteremko

Mzee aomba wahisani wampe sehemu ya kuuzika mwili wa mkewe

T L