• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Ruto akiri kuongoza nchi kama Rais si mteremko

Ruto akiri kuongoza nchi kama Rais si mteremko

NA SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto ameungama haijakuwa rahisi kuongoza nchi, hasa kuimarisha uchumi uliosambaratika.

Dkt Ruto alirithi mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, na serikali yake imekuwa ikilalamika kwamba ilipata hazina ambayo haikuwa na chochote.

Dkt Ruto alisema Jumapili, Desemba 17, 2023 kuwa kinyume na wengi wanavyofikiria kuhusu rais, uongozi si mteremko.

Alisema alifahamu changamoto zinazozingira Amiri Jeshi Mkuu, hata kabla hajachaguliwa kuwa rais 2022.

“Nilipochaguliwa na kuchukua hatamu ya uongozi, nilifahamu haikuwa rahisi, mambo hayangekuwa mteremko,” Rais Ruto alisema kupitia mahojiano ya moja kwa moja na vyombo vya habari, Ikulu, Nairobi.

“Nilijua mambo yangekuwa magumu…Kubadilisha nchi, si sawa na kutembea kwenye bustani,” aliongeza.

Dkt Ruto alichaguliwa Rais 2022 (Kenya Kwanza), kupitia uchaguzi uliokuwa na ushindani mkuu kati yake na kiongozi wa upinzani, Bw Raila Odinga aliyewania kiti hicho cha hadhi ya juu nchini kwa kutumia muungano wa Azimio la Umoja.

Ruto alisaidiwa na mgombea mwenza, Bw Rigathi Gachagua, ambaye kwa sasa ndiye naibu rais, naye Odinga, Bi Martha Karua.

Rais Ruto alizoa kura 7, 176, 141 (sawa na asilimia 50.49 ya kura zilizopigwa) naye Bw Raila Odinga 6, 942,930 (48.85).

Mrengo wa Azimio ulielekea katika Mahakama ya Juu zaidi nchini kupinga matokeo ya kura za urais, japo korti iliharamisha kesi hiyo ikisema haikuwa na ushahidi wa kutosha.

Hoja zote alizoibua Raila, ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri Kkuu, zilifutiliwa mbali.

Dkt Ruto aliapishwa Septemba 13, 2022 na zaidi ya mwaka mmoja baadaye, mengi nchini yamebadilika, ikiwemo nyongeza ya ushuru (VAT) na ada mpya kuzinduliwa.

Rais Ruto anasema Kenya imekuwa ikiahirisha mambo, na ni jukumu lake kuhakikisha nchi inakua.

Dkt Ruto alihudumu kama naibu wa rais chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta (ambaye kwa sasa ni mstaafu).

Bw Kenyatta alitawala kupitia mrengo wa Jubilee.

 

 

 

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ruto: Nilichaguliwa kubadilisha maisha ya Wakenya, si...

Magavana wa eneo la Gusii waonekana kuzima moto wa migogoro...

T L