• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Magavana waweka ‘bet’ yao kwa Raila

Magavana waweka ‘bet’ yao kwa Raila

NA MACHARIA MWANGI

MAGAVANA 30 wametangaza imani yao kwa Raila Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya, wengi wakitarajia hatua hiyo itawasaidia wanaotetea viti vyao kuvihifadhi, huku wanaostaafu na watakaopoteza wakiwa na matumaini kwamba atawakumbuka katika serikali yake iwapo atashinda kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

Hatua hiyo pia inamweka kifua mbele Bw Odinga katika jaribio lake la tano kuingia Ikulu, hasa kutokana na kuwa magavana waliotangaza kuwa nyuma yake wanatoka pembe zote za Kenya.

Bw Javas Bigambo, ambaye ni wakili na mdadisi wa masuala ya siasa anasema kuwa hatua ya magavana hao kuunga mkono Bw Odinga ina manufaa makubwa kwake kwenye uchaguzi ujao.

“Hatua ya magavana 30 kuunga mkono Bw Odinga ina uzito mkubwa kisiasa, kwani itafanya baadhi ya wapigakura ambao hawakuwa na imani naye kubadili nia,” anasema.

WANAOSTAAFU

Bw Bigambo, hata hivyo, anasema kuwa baadhi ya magavana waliotangaza kumuunga mkono Bw Odinga wanahofia kuwa huenda wakashindwa kuhifadhi viti vyao kwa muhula wa pili hivyo kupata nyadhifa serikalini.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba magavana wanaostaafu wameamua kuunga mkono Bw Odinga kutokana na imani kwamba atashinda urais, hivyo kuwateua serikalini. Wanajipanga ili wasijipate kwenye baridi ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Watakaoshindwa pia wana matumaini sasa,” anasema Bw Bigambo.

Magavana wanaostaafu ambao ushindi wa Bw Odinga unaweza kuwa baraka kwao kwa kutunukiwa vyeo ni Kivutha Kibwana (Makueni), James Ongwae (Kisii), Cyprian Awiti (Homa Bay), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), Martin Wambora (Embu), Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi), Cornel Rasanga (Siaya) na Wycliffe Oparanya (Kakamega).

KARATA YA ODINGA

Walio na matumaini kuwa karata ya Bw Odinga huenda ikawafaa kuhifadhi vyeo vyao ni Charity Ngilu (Kitui), Lee Kinyanjui (Nakuru), Anyang Nyong’o (Kisumu), Wilberforce Otichilo (Vihiga), Wycliffe Wangamati (Bungoma) na Ndiritu Muriithi (Laikipia).

Wengine wanaotarajia kufaidi kubakia madarakani kwa msisimko wa Bw Odinga ni James Nyoro (Kiambu), Mohamed Kuti (Isiolo), Ali Korane (Garissa), Anne Kananu (Nairobi), Granton Samboja (Taita Taveta), Fahim Twaha (Lamu), Francis Kimemia (Nyandarua), Amos Nyaribo (Nyamira), Joseph ole Lenku (Kajiado) na Dhadho Godhana (Tana River).

Akisoma taarifa ya magavana walioamua kupiga Bw Odinga jeki, Gavana Muriithi alisema Afred Mutua wa Machakos, Kiraitu Murungi wa Meru na John Lonyagapuo wa Pokot Magharibi pia wameazimia kuwa katika mrengo wa Azimio la Umoja, ingawa hawakuweza kuhudhuria kikao cha jana mjini Naivasha.

Magavana hao walisema Bw Odinga ana sifa ya kuleta mabadiliko nchini na kulinda ugatuzi: “Tumekutana na Bw Odinga leo kumhakikishia kuwa tutasimama naye hadi mwisho.”

Prof Kibwana alitangaza kutupilia mbali azma yake ya kutaka kuwania urais na badala yake ataunga mkono Bw Odinga: “Baada ya kushauriana na watu wa Makueni, walinieleza kwamba umri wangu bado ni mdogo na ninafaa kuunga mkono Raila ambaye ana tajriba kubwa katika masuala ya uongozi.”

Bw Lenku alisema kuwa magavana hao sasa wataanza mbio za kumsaidia Bw Odinga kusaka kura kote nchini: “Sisi sasa ni wanajeshi wako na tutakuvumisha kuanzia ngazi ya vijijini.”

Gavana Tolgos alisema kuwa vuguvugu la Azimio la Umoja linaloongozwa na Bw Odinga lina uungwaji mkubwa hata katika eneo la Bonde la Ufa, ambayo ni ngome ya mpinzani wake mkuu, Naibu Rais William Ruto.

BONDE LA UFA

“Katika mkutano wetu pia tulijadili suala la usalama katika eneo la Bonde la Ufa na Bw Odinga aliahidi kuhakikisha kuwa kuna amani katika kaunti zinazoandamwa na visa vya ukosefu wa usalama,” akasema Bw Tolgos.

Bw Odinga alisema yuko tayari kuongoza nchi iwapo atachaguliwa kuwa rais.

“Magavana wana tajriba kuhusu ugatuzi, hivyo kuniunga mkono kwao kuna manufaa makubwa kwangu,” akasema Bw Odinga.

Alisema kuwa atatengea kaunti kiasi kikubwa cha fedha iwapo atachaguliwa kuwa rais na akamshambulia Dkt Ruto kwa kujaribu kuleta mgawanyiko baina ya matajiri na maskini.

  • Tags

You can share this post!

Hofu rangi za tattoo zasababisha kansa

Siku ya sarakasi kwa Wanjigi, alala ndani licha ya...

T L