• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:36 PM
Majukumu ya AG yagawiwe Waziri – Korti

Majukumu ya AG yagawiwe Waziri – Korti

Na JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA Kuu imemwaagiza Rais Uhuru Kenyatta kuteua Waziri mahsusi atakayetekeleza baadhi ya majukumu yanayotekelezwa sasa na Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki.

Jaji James Makau alimtaka Rais Kenyatta kumtwika Waziri, anayefaa, majukumu ya kutekeleza sheria sita zinazoongoza utendakazi wa mashirika mbalimbali ya serikali na Afisi za Kikatiba.

Jaji Makau alieleza kuwa kwa kuweka wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo chini ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Rais anahujumu malengo ya sheria hizo pamoja na masilahi ya umma.

Alisema hayo alipotoa uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa mahakamani na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kupinga hatua ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kusimamia mashirika ya serikali.

LSK iliambia mahakama kuwa sheria hizo zilianza kutekelezwa baada ya Rais Kenyatta kutangaza mabadiliko katika uendeshaji wa serikali kupitia Amri Kuu Nambari 1 ya 2018.

Sheria hizo sita ni pamoja na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Ndogo, Sheria ya Mafunzo ya Uanasheria, Sheria kuhusu Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria, Sheria ya Idara ya Mahakama, Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu na Sheria ya Kulinda Waathiriwa wa Dhuluma.

Katika uamuzi huo ambao ni pigo kwa Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki, “ni wajibu wa Kikatiba wa Rais kuteua na kuwapa majukumu Mawaziri inavyopaswa ili watekeleze Sheria zote zilizoundwa na Bunge.”

Kwa hivyo, Jaji Makau alisema kuwa wajibu wa kutekeleza sheria hizo hauwezi kutwikwa Mwanasheria Mkuu kwa sababu yeye si Waziri, kulingana na kipengee cha 132 (3) cha Katiba.

Aidha, katika maelezo kuhusu namna sheria hizo zinavyopaswa kutekelezwa, afisi inayorejelewa ni ya Waziri wala si ile ya Mwanasheria Mkuu.

“Kulingana na sheria zinazotungwa na bunge, iwapo kuna nia ya kurejelea Mwanasheria Mkuu kama Waziri, ufafanuzi huo hutolewa moja kwa moja na kwa njia iliyo wazi,” akasema Jaji Makau, alipokuwa akirejelea sheria tatu ambapo Mwanasheria Mkuu amerejelewa kama “Waziri”.

Alisema Rais Kenyatta alivunja Katiba, na kukiuka hitaji la utawala wa sheria, kwa kutoteua Waziri mahususi atakayesimamia utekelezaji wa sheria hizo.

“Nimebaini kuwa mlalamishi ameonyesha Rais alifeli kuzingatia wajibu wake kulingana na kipengee cha 132 (3) cha kuteua Mawaziri kulingana na lengo la sheria husika.” Jaji Makau akasema.

“Ni muhimu kuzingatia kwamba katika sheria wajibu wa Waziri ni muhimu. Hujumuisha usimamizi na utekelezaji wa sheria zilizotungwa na Bunge,” akaeleza.

Akipinga kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto, alisema Katiba inampa Rais mamlaka ya kuongoza na kushirikisha majukumu ya wizara na idara za serikali.

Lakini Jaji Makau alimwambia kuwa japo Rais ana wajibu wa kugawa majukumu hayo, sharti wajibu huo utekelezwe bila kukiuka Katiba.

“Asipofanya hivyo, utekelezaji wa wajibu huo unaweza kubatilishwa,” akaeleza.

You can share this post!

Shule zafungwa Addis wanafunzi wavune mazao ya...

IEBC kufanya usajili tena Januari 2022

T L