• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mapinduzi ya Jubilee, raha Kenya Kwanza

Mapinduzi ya Jubilee, raha Kenya Kwanza

MERCY KOSKEI Na ALEX NJERU

WANDANI wa Rais William Ruto walisherekea mapinduzi yaliyotekelezwa katika chama cha Jubilee jana Ijumaa ambapo Katibu Mkuu Jeremiah Kioni na Naibu Mwenyekiti David Murathe walivuliwa nyadhifa hizo.

Kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, Seneta wa Nandi Samson Cherargei, na mbunge wa Belgut Nelson Koech ni miongoni mwa waliosherehekea kutimuliwa kwa wawili hao.

“Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee linastahili pongezi tele kwa kuwatimua Kioni na Murathe ambao walikuwa wakirudisha nyuma chama hiki cha Jubilee kwa kukihusisha na maandamano. Aidha, Jubilee imefanya vizuri kwa kuanza mchakato wa kuondoka Azimio,” akasema Bw Cherargei kwa Twitter.

Kwa upande wake, Bw Cheruiyot alimpongeza Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega kwa kuteuliwa kuwa kaimu Katibu Mkuu.

“Pongezi ndugu yangu Bw Kega. Japo mimi niko ndani ya UDA, mimi ni mwenye hisa, daraja ya A, katika Jubilee. Inatukera kwamba mwendawazima alihudumu kama katibu mkuu,” akasema Seneta huyo wa Kericho.

Katika mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee (NEC) uliongozwa na mwenyekiti Nelson Dzuya, Bw Kioni na Murathe walitimuliwa. Mweka Hazina wa kitaifa Kagwe Gichohi pia alitimuliwa.

Bw Kega aliteuliwa kuwa kaimu Katibu Mkuu huku Mbunge wa Eldas, Adan Keynan akichaguliwa kuwa kaimu Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa. Mbunge wa Kitui Kusini, Rachel Nyamai sasa ndiye atakayehudumu kama kaimu Mweka Hazina.

“Chama cha Jubilee kimemsimamisha kazi Jeremiah Kioni (Katibu Mkuu), Mweka Hazina Kagwe Gichohi na Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa David Murathe. Maafisa hao wamesimamishwa mara moja na kesi zao zimewasilishwa kwa asasi ya kusuluhusisha mizozo ndani ya chama,” ikasema taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo uliofanyika katika mkahawa wa Sarova Woodlands Hotel, Nakuru.

Baraza hilo pia liliamua kuwa chama hicho kiandae kongamano maalum la wajumbe ndani ya miezi sita huku likianza mchakato wa kujiondoa muungano wa Azimio la Umoja-One.

“Kabla ya kuandaliwa kwa kongamano la wajumbe, Baraza Kuu la Kitaifa litaanza mchakato wa kuondoka Azimio. Kamati hiyo itafanya mazungumzo na muungano wa Kenya Kwanza kuhusu uwezekano wa kubuni ushirikiano,” taarifa hiyo pia ikaongeza.

Lakini Bw Kioni amepuuzilia mbali kutimuliwa kwake akisisitiza kuwa bado ndiye Katibu Mkuu wa chama alichosisitiza kuwa kingali ndani ya Azimio.

Akiongea katika mkutano wa hadhara wa Azimio katika eneo la Mlolongo, Machakos, alimshtumu Rais Ruto kwa kudhoofisha upinzani kwa kuwanunua wabunge wake.

“Wale walionunuliwa katika Ikulu ili wavunje Azimio walifanya kazi bure. Jubilee ingali ndani ya Azimio. Mimi ndiye Katibu Mkuu na Uhuru Kenyatta ndiye kiongozi wetu. Wale walionunuliwa wakaenda Ikulu ndio wanafaa kuondoka,” akasema.

Bw Kioni alisema wale wanaopasa kuhama Jubilee ni Bw Kega, Mbunge Maalum Sabina Chege, David Kiaraho (Ol Kalou), Irene Njoki (Bahati), Zachary Kwenya (Kinangop), Shadrack Mwiti ( Imenti Kusini), Mark Mwenje (Embakasi Magharibi), Amos Mwago (Starehe), Dan Karitho (Igembe ya Kati), Stanley Muthama (Lamu West), Joseph Githuku (seneta Lamu), Omar Shurie (Balambala) na John Waluke (Sirisia), miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Ukame kusukuma bei ya umeme juu – Waziri

Wito EAC itume wanajeshi zaidi kukabili waasi DRC

T L