• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Wito EAC itume wanajeshi zaidi kukabili waasi DRC

Wito EAC itume wanajeshi zaidi kukabili waasi DRC

NA MASHIRIKA

BUJUMBURA, BURUNDI

MATAIFA wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yametakiwa kutuma wanajeshi zaidi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupambana na waasi wa M23 na kulinda raia.

Kwenye taarifa ya kwanza aliyotoa Alhamisi, siku tano baada ya kukamilika kwa mkutano wa marais wa nchi za EAC jijini Bujumbura, Burundi, mpatanishi mkuu wa mchakato wa kuleta amani DRC Uhuru Kenyatta, alisema wanajeshi wanafaa kusaidia kukomboa maeneo ya mashariki mwa DRC yaliyotekwa na waasi wa M23.

Waasi hao wamekuwa wakipigana na wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo tangu mwaka jana.

“Mpatanishi mkuu anatoa wito kwa mataifa yaliyochangia wanajeshi katika kikosi cha wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) kuongeza wanajeshi zaidi katika eneo lote la mashariki mwa DRC, haswa mkoa wa Kivu Kaskazini. Wanajeshi hao wafaa kushika doria katika maeneo yaliyokombolewa na kuingia katika maeneo ambayo yangali yametekwa na waasi,” Bw Kenyatta, ambaye ni Rais mstaafu wa Kenya, akasema kwenye taarifa.

Hata hivyo, kiongozi huyo hakuhudhuria mkutano huo wa marais wa EAC uliofanyika Jumamosi wiki jana, akitaja changamoto za usafiri na notisi fupi iliyotolewa.

Lakini Bw Kenyatta alisema alikubaliana na maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wa jumuiya ya EAC waliotaka mapigano yasitishwe, waasi waondoke na wakuu wa vikosi vya wanajeshi watoe makataa ya waasi hao kuondoka.

Wito wa Bw Kenyatta wa kuongezwa kwa wanajeshi wa EACRF unaashiria kuwa anaunga mkono kikosi hicho kilichoundwa mwaka jana kusaidia katika kuleta amani DRC.

Lakini kikosi cha EACRF kimekabiliwa na pingamizi kubwa jijini Goma huku raia wakiwalaumu wanajeshi hao kwa kushindwa kuwafurusha waasi wa M23.

Aidha, wananchi hao pia wanataka wanajeshi wa DRC waruhusiwe kusimamia usalama katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa udhibiti wa waasi.

Vile vile, mataifa mengine yanayochangia wanajeshi katika EACRF kama vile Sudan Kusini na Uganda yametangaza mipango ya kuongeza idadi ya wanajeshi. Lakini hadi wakati huu, wanajeshi hawajatumwa DRC.

Wanajeshi wa Sudan Kusini wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa maafisa wa DRC.

Uganda na Burundi zilikuwa zimetuma wanajeshi chini ya mpango wa maelewano na DRC.

Bw Kenyatta anasisitiza kuwa wanajeshi wa EACRF watumwe kulinda raia na kuzuia vita kati ya wapiganaji wa M23 na wanajeshi wa DRC (FARDC).

Kufikia sasa ni wanajeshi wa Kenya pekee katika EACRF wako jijini Goma lakini hawajaingia katika eneo la vita.

Wakati huo huo, jana Ijumaa raia walitoroka makwao katika na mji wa Goma baada ya hofu kutanda kwamba wapiganaji wa M23 wanakaribia.

Kumekuwa na ripoti kwamba wanajeshi wa DRC wamekuwa wakipigana na waasi hao karibu na mji wa Sake.

Maelfu wamehama makazi yao katika miezi ya hivi karibuni baada ya waasi hao wa kabila la Tutsi kutekeleza mashambulio.

  • Tags

You can share this post!

Mapinduzi ya Jubilee, raha Kenya Kwanza

DOUGLAS MUTUA: Waombeeni wasanii wa injili waziepuke kashfa...

T L