• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
‘Mayatima’ wa Raila wabaki kwa mataa

‘Mayatima’ wa Raila wabaki kwa mataa

NA VALENTINE OBARA

BAADHI ya wanasiasa waliokuwa wakisubiri kupewa vyeo vya juu serikalini endapo Kinara wa ODM Raila Odinga angeshinda urais, wamebaki mataani baada ya Mahakama ya Upeo kuthibitisha ushindi wa William Ruto.

Wanasiasa hao wanajumuisha magavana waliokamilisha mihula miwili ya uongozi, mawaziri wa serikali ya rais anayeondoka Uhuru Kenyatta, na wanasiasa waliotaka kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi wa Agosti 9, lakini wakashawishiwa kuachia wenzao nafasi.

Huku hatima ya wengi waliotarajia kupata nafasi ndani ya serikali ya Azimio ikiwa katika njia panda, imebainika huenda baadhi yao wakahamia upande wa Kenya Kwanza.

Kufikia jana Jumanne, wengi wa waliokuwa na matumaini ya kuteuliwa serikalini walikuwa hawajatamka chochote kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Upeo.

Katika mipangilio ya Azimio, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa ameahidiwa wadhifa wa kinara wa mawaziri.

Kwa kuona mambo yameenda mrama, Bw Kalonzo alichukua karatasi za kuomba kazi ya spika wa bunge la kitaifa.

Magavana wanaoondoka Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) walikuwa pia wameahidiwa nafasi za uwaziri kama Azimio ingeshinda urais.

Bw Joho aliahidiwa cheo cha waziri wa ardhi huku Bw Oparanya akitengewa wizara ya fedha.

Mbali na hao, kuna wanasiasa ambao waliamua kutowania nyadhifa zozote kwa ahadi kuwa watateuliwa kwenye serikali ya Bw Odinga.

Wanajumuisha Suleiman Shahbal, ambaye alitaka kuwania ugavana Mombasa, Kenneth Marende aliyeweka kando azma yake ya kuwania ugavana wa Vihiga na mwenyekiti wa ODM, John Mbadi, aliyekubali kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Homa Bay.

Aliyekuwa gavana wa Kitui, Charity Ngilu naye aliamua kutotetea kiti chake.

Bw Marende aliahidiwa wadhifa wa Spika wa Seneti huku Bw Mbadi na Bi Chege wakiwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa wabunge maalumu.

Mawaziri katika serikali ya Rais Kenyatta waliotarajia kuteuliwa katika serikali ya Bw Odinga ni James Macharia (Uchukuzi), Joe Mucheru (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), Keriako Tobiko (Mazingira), Ukur Yatani (Fedha), Mutahi Kagwe (Afya) na Fred Matiang’i (Usalama).

Wengine ni Eugene Wamalwa (Ulinzi), Peter Munya (Kilimo) na Raphael Tuju.Wengine waliokuwa wakitegea vyeo vya juu katika serikali ya Azimio ni waliokuwa magavana Nderitu Muriithi (Laikipia), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet), Mwangi wa Iria (Murang’a) na James Ongwae wa Kisii.

Ushindi wa Dkt Ruto pia ni pigo kwa mabwanyenye na viongozi wa mashirika ya kijamii ambao waliunga mkono Azimio akiwemo Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, na aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth.

Vilevile, mamia ya wanasiasa ambao wamejijenga kisiasa kwa msingi wa kumuunga mkono Bw Odinga kila wakati wa uchaguzi huenda wakalazimika kuunda mikakati upya.

Hii ni kutokana na kuwa, akiwa na umri wa miaka 77 sasa, uwezekano wa Bw Odinga kuwania urais tena ifikapo 2027 ni finyu kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa.

“Raila huwania ili ashinde urais lakini kuna watu wamemzunguka kwa nia ya kujinufaisha kibinafsi. Hawajali kama atashinda au la, na hivi sasa wanamwandaa kwa uchaguzi wa 2027. Lazima ‘Baba’ aangalie nyuma na ajue wandani wake wanaojifanya kummiliki wanajinufaisha kibinafsi,” akasema mchanganuzi wa siasa, Arnold Maliba.

Katika baadhi ya maeneo ya nchi ambapo Bw Odinga ana ufuasi mkubwa, mshindi wa tikiti ya kuwania wadhifa wa kisiasa kupitia Chama cha ODM huchukuliwa kama tayari ashakuwa mshindi.

Hii ilithibitishwa katika uchaguzi wa Agosti 9, katika kaunti ambazo ODM ilizoa viti vingi vya kisiasa ikilinganishwa na vyama vingine.

  • Tags

You can share this post!

Real Madrid waanza kutetea ufalme wa UEFA kwa ushindi dhidi...

Rais mteule azungumza na Rais anayestaafu

T L