• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Mbogo awasuta wapinzani wake Mombasa

Mbogo awasuta wapinzani wake Mombasa

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, amewasuta wapinzani wake kwenye kinyang’anyiro cha ugavana Kaunti ya Mombasa, akisema kaunti hiyo inahitaji mabadiliko bora ya kimawazo katika uongozi.

Bw Mbogo alidai kuwa, utawala wa Gavana Hassan Joho haukufanikisha maendeleo Mombasa kwa kiasi cha kuridhisha ikizingatiwa kiwango cha fedha za ugatuzi kilichotoka kwa serikali ya kitaifa.

Bw Mbogo alieleza kuwa, amethibitisha uongozi bora wa kuleta maendeleo kama vile kwa kujenga shule na barabara eneobunge la Kisauni tangu alipochaguliwa mwaka wa 2017.

Anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, na mfanyabiashara Suleiman Shahbal wanaoshindania tikiti ya ODM, na aliyekuwa seneta Hassan Omar ambaye anatarajiwa kuwania kiti hicho kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

“Wametutawala kimawazo, kifikra na kiuchumi, tutaendelea kuwa maskini na wataendelea kututawala. Wakati umefika kukataa utumwa. Lazima mujihusishe kwenye vita hivi,” alisema.

Bw Mbogo anatarajia kuwania kiti hicho kupitia kwa Chama cha Wiper.

Kwingineko, Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, amewasihi wakazi wa eneo bunge lake kumuunga mkono kwenye azma yake ya kuhifadhi kiti chake.

Bi Mboko alisema tangu achaguliwe mbunge amefanikisha miradi ya maendeleo katika sekta tofauti ikiwemo elimo, usambazaji maji, usalama, miongoni mwa nyingine ambazo anaamini zinampa nafasi bora ya kuaminiwa na wapigakura katika uchaguzi ujao.

Bi Mboko ambaye amedaiwa kuwa mmoja wa wanasiasa wanaotarajiwa kupewa tikiti ya moja kwa moja katika Chama cha ODM, alisema anataka kurudi bungeni kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakazi wake.

“Ninaomba kura zenu, mnichague nikamilishe maendeleo katika masuala ya elimu, miundomsingi hasa barabara na usalama,” akasema.

Mbunge huyo ameshikilia kiti hicho kwa kipindi kimoja tangu mwaka wa 2017. Katika uchaguzi wa 2013, alifanikiwa kuwa mbunge mwakilishi wa kike wa kwanza katika Kaunti ya Mombasa.

You can share this post!

Katibu mkuu ashtakiwa kumzaba mkewe makonde akiwa na mimba

Mchujo: Shahbal, Nassir walumbania tiketi ODM

T L