• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Mbogo kudai ‘nusu mkate’ kwa Sonko

Mbogo kudai ‘nusu mkate’ kwa Sonko

NA FARHIYA HUSSEIN

MBUNGE wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, amefafanua atataka mgao sawa wa mamlaka kati yake na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, iwapo watashinda ugavana katika Kaunti ya Mombasa.

Bw Mbogo alikubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko kupitia Chama cha Wiper katika uchaguzi wa Agosti, baada ya Wiper kufutilia mbali cheti cha muda alichokuwa amepewa kuwania nafasi hiyo.

“Nina uwezo na haki ya kutoa maamuzi kama yeye. Atapata nusu ya mamalaka na mimi nusu nyingine. Ninapotaka kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara, haitakuwa lazima kwangu kuomba ruhusa yake (Sonko) kwa sababu itakuwa wajibu wangu kama naibu gavana,” akasema Bw Mbogo.

Lengo la Bw Sonko kuwania ugavana Mombasa bado linakumbwa na pingamizi kutoka kwa pande tofauti.

Jumanne, mashirika ya kijamii Mombasa yalisema yanapanga kuwasilisha kesi mahakamani ili kumzuia kuwania kiti hicho kwa msingi kuwa alitimuliwa mamlakani Nairobi kwa sababu ya ufisadi.

Kesi nyingine sawa na hiyo iliwasilishwa mahakamani wiki chache zilizopita, na bado inasubiriwa kuendelea.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilikuwa imesema haiwezi kumzuia mwanasiasa kuwania kiti ikiwa amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa kutimuliwa mamlakani.

“Kama IEBC haina ujasiri wa kufanya maamuzi kuhusu masuala ya kimaadili, basi tutapeleka kesi wenyewe mahakamani,” akasema mwanaharakati, Kasisi Gabriel Dolan.

Endapo Bw Sonko ataidhinishwa kuwania urithi wa kiti cha Gavana Hassan Joho, atapambana na Bw Abdulswamad Nassir (ODM), Bw Hassan Omar (UDA), na Dkt William Kingi (PAA) miongoni mwa wengine.

Wakati huo huo, Bw Mbogo pia alimshutumu Bw Nassir akidai kuwa hatatatua matatizo ya wakazi wa Mombasa bali ataendeleza utawala ulioshuhudiwa wakati wa uongozi wa Bw Joho.

Akizungumza katika eneo la Jomvu, alisema akishirikana na Bw Sonko serikali yao itaangazia kusuluhisha tatizo la kudumu la uchafu na uhaba wa maji.

“Uhaba wa maji umekuwa tatizo kubwa kwa wakazi wetu. Tuna maji ya bahari na tutahakikisha tunatekeleza mradi wa kusafisha maji ya chumvi na kugeuza kuwa maji safi ili kuhakikisha wakazi wanapata maji kwenye mabomba yao,” akasema Bw Mbogo.

Bw Sonko alizindua kampeni zake za ugavana Mombasa wikendi iliyopita, ila walizuiwa kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja mkubwa wa Tononoka ikidaiwa hapakuwa na maandalizi bora ya usalama.

Mwenyekiti wa Wiper tawi la Mombasa, Sheikh Twaha Omar alilalamika kwamba hatua hiyo inaashiria siasa chafu kutoka kwa baadhi wa viongozi wa kaunti.

“Tulikuwa tumelipia uwanja huo, hatuelewi utaratibu uliotumika kutukataza. Sisi ni familia moja chini ya muungano wa Azimio na tungempigia debe Bw Raila Odinga katika azma yake ya kuwania urais,” akasema Bw Omar.

  • Tags

You can share this post!

Lamu: Wachuuzi kurudishwa ndani katika soko la manispaa...

Ombi mradi wa kilimo ulioanzishwa na Kibaki urejeshwe Kilifi

T L