• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Mbunge ataka wapewe uhuru kubadilisha hoja za Rais katika miswada

Mbunge ataka wapewe uhuru kubadilisha hoja za Rais katika miswada

Na CHARLES WANYORO

MBUNGE wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood amependekeza katiba ifanyiwe mabadiliko kuhusiana na idadi ya wabunge wanaohitajika kubatilisha hatua ya Rais kukataa kutia saini miswada.

Kwa sasa, katiba inahitaji thuluthi mbili ya wabunge kubadilisha hatua hiyo. Akizungumzia hatua ya Rais iliyopendekeza ushuru wa kuongeza thamani (VAT) kwa mafuta, mbunge huyo alisema haikuwa rahisi kwa wabunge 233 kufika bungeni kwa wakati mmoja kubatilisha pendekezo.

Bw Dawood aliwaondolea wabunge lawama kuhusiana na ongezeko la bei ya mafuta, akisema wale waliokuwa bungeni wakati huo walipinga pendekezo hilo lakini hawakufikisha idadi hitajika ya 233.

Alisema ushuru huo wa VAT unawaumiza wananchi ambao bado wanaathirika na makali ya janga la Covid-19.

Mbunge huyo ambaye alihudumu kama mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, alisema wabunge waliwahi kufikisha idadi hiyo ya 233 katika kikao kimoja wakati wa mjadala kuhusu mswada wa BBI.

“Katiba ikifanyiwa marekebisho miaka ijayo, kipengele hicho kiondolewe kwa sababu marais wamekuwa wakikitumia kuhujumu mamlaka ya wabunge katika uundaji wa sheria,” akasema Bw Dawood.

Mbunge huyo alikuwa akiwatuhutubia wakazi aliposambaza hundi za thamani ya Sh5 milioni za pesa za Hazina ya Uwezo.

Alisema Mswada wa Fedha wa 2018 ulilenga kuanzisha ushuru wa VAT wa kiwango cha asilimia 16 lakini wabunge wakalalamika na ndipo ukapunguzwa hadi asilimia nane.

Mswada huo pia ulipendekeza kuwa mafuta taa yatozwe ushuru wa Sh18 kwa lita ili kuzuia wafanyabiashara walaghai kuyachanganya na dizeli.

You can share this post!

Ruto kutua Kisii kuzima ushawishi wa Matiang’i

Ni makosa UN kuzitenga nchi zilizo na misukosuko