• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Mbunge wa ‘Kieleweke’ anayetumia kila mbinu kuhakikisha Ruto hataingia Ikulu 2022

Mbunge wa ‘Kieleweke’ anayetumia kila mbinu kuhakikisha Ruto hataingia Ikulu 2022

Na PETER MBURU

NDIYE alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka eneo la Mlima Kenya na wa chama cha Jubilee kudai kuwa jamii ya eneo hilo haitamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kugombea Urais mnamo 2022.

Hata kabla ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuzika tofauti zao kisiasa na kutuliza nchi wakati vurugu zilizidi mwaka jana, Ngunjiri Wambugu-mbunge wa Nyeri Mjini alikuwa ameanza vita na Dkt Ruto.

Akitoa matamshi hayo awali Januari 2018, miezi michache tu baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge, Bw Wambugu alisema Dkt Ruto hafai kuwa na uhakika sana kuwa Mlima Kenya utamuunga mkono.

Watu wengi, hata hivyo, walimpuuza kuwa aliyekuwa akitafuta umaarufu na hata viongozi wa eneo hilo wakajitokeza kwa haraka kutuliza hali, kwa kuhakikishia Naibu Rais kuwa kura za eneo hilo ni zake katika uchaguzi ujao.

Lakini Bw Wambugu, mwanaharakati, mwanafunzi wa siasa na mwandishi mpevu, hakuachia hapo kwani tangu wakati huo amekuwa akimshambulia Dkt Ruto kila wakati, kumkosoa kwa takriban kila jambo na hata akaanzisha vuguvugu liitwalo ‘Kitaeleweka’, ambalo sasa linavuma na kumkosesha Naibu Rais usingizi.

Huenda wengi walimpuuza alipoanza, lakini kadri jinsi muda umekuwa ukisonga, vuguvugu lake limekuwa likipata nguvu na uungwaji mkono, sasa likiwa na sehemu ya viongozi kutoka Mlima Kenya na Bonde la Ufa ambao wanaliunga mkono.

Kazi ya Kitaeleweka ni kutaja makosa ya Naibu Rais ama popote anapohusishwa na mambo ya kumchafulia jina, kisha kusema kuwa yataangaziwa mnamo 2022 kuwafanya Wakenya wasimchague.

Bw Wambugu na kundi lake wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto kuwa anaendesha kampeni za mapema kujitafutia umaarufu kabla ya 2022, hali wanayosema inalemaza juhudi za Rais Kenyatta kutekeleza ajenda zake kwa wananchi.

“Hatuna viongozi wawili katika Jubilee, tuna mmoja. William Ruto hana kazi yoyote yake isipokuwa zile anazopewa na Rais. Kwa hivyo, ukiniambia nimuunge mkono, unaniambia nimuunge mkono kufanya nini? Ikiwa namuunga mkono Rais, hiyo ni kumaanisha namuunga mkono naibu wake, lakini tu ikiwa anafanya kulingana na maagizo ya Rais,” mbunge huyo alisema majuzi.

Huu ndio umekuwa msimamo wake, kuwa Dkt Ruto anamkosea Rais heshima, kila wakati akiwa mstari wa mbele kumkosoa.

Ni kiongozi mwenye ujuzi wa kutumia mitandao ya kijamii kupitisha ujumbe, hali ambayo imemfanya kutumia akaunti zake za Facebook na Twitter kila wakati kuvumisha vuguvugu lake la Kitaeleweka.

Bw Wambugu huwa hachelei kumpiga Naibu Rais kisiasa kila fursa inapojitokeza.

“Wakati unavamia handisheki ukiwa wa kutoka Jubilee, mtu unayemvamia ni Uhuru Kenyatta kwani handisheki ilikuwa yake nusu, na ya Raila nusu,” akasema akirejelea Dkt Ruto.

Na kwa namna moja ama nyingine ujasiri wake na athari ambazo umesababisha Mlimani umemfanya kupata marafiki na maadui, hata Dkt Ruto akijipata kumjibu katika mikutano ya hadhara.

Kwa sasa, vuguvugu la Kitaeleweka limevutia viongozi mbalimbali, waliochaguliwa ama wa zamani, ambao wanatofautiana na Dkt Ruto, ndani na nje ya Mlima Kenya.

Wabunge kama Maina Kamanda (Maalum), Muturi Kigano (Kangema), Paul Koinange (Kiambaa) na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, pamoja na wengine tayari wameunga mkono vuguvugu hilo na kuanza kutoa wito kuwa eneo la Mlima Kenya halitampigia kura Dkt Ruto.

Hii ni licha ya viongozi wengine kutoka Bonde la Ufa ambao wanatofautiana na Naibu Rais kama mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny, na viongozi wa chama cha KANU.

Wafuasi wa Dkt Ruto aidha sasa wanatumia kila mbinu kuvamia kundi hilo, ambalo nguvu zake zinapenyeza ndani ya Jubilee na kujiweka kama chaguo la viongozi wote wanaotofautiana na Dkt Ruto.

Mbunge huyo, ambaye alikuwa mwanachama wa ODM kati ya 2012 na 2017 amekuwa akilaumiwa na wafuasi wa Dkt Ruto kuwa anatumiwa na chama hicho kuvuruga Jubilee, lakini yeye anasisitiza kuwa anamtetea Rais Kenyatta.

Akianza hakuwa na upinzani mkubwa, wala uungwaji mkono wowote, lakini jinsi anavamiwa na kuungwa viongozi mashuhuri kwa sasa ni ishara tosha kuwa kile alichoanzisha kinawanyima wengi usingizi, na ishara kuhusu makabiliano yanayosubiriwa mbele.

You can share this post!

Raha ya ndoa ni kutogawa asali, utafiti wathibitisha

Mashetani Wekundu wazikwa na Everton

adminleo