• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Miamba wabwagwa mchujoni

Miamba wabwagwa mchujoni

NA WAANDISHI WETU

WANASIASA wenye uzoefu mkubwa na washiriika wa Naibu Rais William Ruto ni miongoni mwa waliobwagwa katika kura za mchujo wa chama United Democratic Alliance (UDA).

Wanasiasa hao sasa watalazimika kuwania kama wagombea wa kujitegemea au kungojea kuteuliwa serikalini iwapo Dkt Ruto atashinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Aliyekuwa Waziri wa Kawi, Charles Keter, Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Cheboi na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, Caleb Kositany ni miongoni mwa vigogo walioangushwa na wanasiasa limbukeni katika kura hiyo iliyofanyika Alhamisi.

Bw Keter, ambaye amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Belgut kwa mihula miwili na seneta wa Kericho kwa miaka miwili, alibwagwa na mhadhiri wa chuo kikuu, Dkt Eric Mutai katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kericho.

Tulipokuwa tukienda mitamboni, Dkt Mutai ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Embu alikuwa akiongoza kwa idadi ya kura kutoka maenebunge matano kati ya sita katika kaunti hiyo ya Kericho.

Bw Cheboi alishindwa kutamba baada ya kushindwa na diwani wa sasa wa wadi ya Sirikwa, Alfred Mutai aliyejipatia kura 17, 247 huku Cheboi akizoa kura 12,454 pekee.

Bw Mutai ni mwanasiasa limbukeni ambaye kabla ya kujitosa katika siasa, alijipatia riziki kupitia biashara ya makaa.

Katika kaunti ya Uasin Gishu, juhudi za Bw Kositany, ambaye pia ni mshirika wa karibu wa Naibu Rais, za kupata tikiti ya UDA kuwania kiti cha ugavana ziliambulia patupu baada ya kushindwa na mwanasiasa Jonathan Bii.

Wengine waliowania tikiti hiyo ni mabalozi wa zamani Julius Bitok (Pakistan) na Sarah Serem (China), aliyekuwa waziri katika serikali ya kaunti ya Nairobi Vesca Kangogo na mfanyabiashara David Singoei.

Bw Bii, maarufu kama “Koti Moja” alizoa jumla ya kura 71,152 akifuatwa kwa karibu Bw Bitok aliyepata kura 59,001.

Wabunge wengine wandani wa Dkt Ruto ambao hawakufaulu kupata tiketi ya UDA kutetea viti vyao ni David Rono (Keiyo Kusini), Cornelly Serem (Aldai), James Murgor (Keiyo Kaskazini), Jane Kihara (Naivasha) na Mbunge Mwakilishi wa Kike, Laikipia, Catherine Waruguru ambaye alikuwa akisaka tiketi ya chama hicho kuwania kiti cha ubunge cha Laikipia Mashariki.

Bw Serem alibwagwa na aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi katika Afisi ya Naibu Rais Maryanne Kaitany katika kinyang’anyiro kikali. Bi Kaitany alipata kura 16,597 dhidi ya 13, 878 alizopata mbunge huyo.

Naye Bi Wairuguru ambaye amekuwa mtetezi sugu wa Dkt Ruto alishindwa pale alipopata kura 5, 595 nyuma ya Mbunge wa sasa wa Laikipia Mashariki, Amin Deddy Mohamed aliyepata kura 12,748.

Katika kaunti hiyo hiyo, juhudi za Mbunge wa Laikipia Magharibi Patrick Mariru za kutwaa tiketi ya UDA kuwania ugavana zilifeli baada ya kushindwa na Gavana wa zamani, Joshua Irungu.

Bi Mariru, ambaye ni Spika wa zamani wa Bunge la kaunti hiyo, pia alihudumu kama spika wa muda katika Bunge la Kitaifa.

Seneta wa sasa wa Bomet, Dkt Christopher Langat na Mbunge Maalum Wilson Sossion walitishia kujiondoa kutoka UDA baada ya kubwagwa na wakili Hillary Sigei.

Wakiongea na wanahabari mjini Bomet jana, walitaja wakuu wa UDA kama “kundi la wezi.” “Katu hatutapiga magoti mbele ya uongozi wa chama hicho. Mchujo huu umeendeshwa katika njia inayohujumu demokrasia ambayo UDA inadai kuendeleza,” akafoka Bw Sossion, ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut).

Lakini wawili hao walipokuwa wakilalamika kuwa mchujo huo haukuendeshwa kwa njia huru na haki, aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Miundo Msingi Dkt John Mosonik alikubali kushindwa na Gavana wa sasa, Hillary Barchok.

Sasa Bw Barchok ndiye atapeperusha bendera ya UDA kukabiliana na Gavana wa zamani Isaac Ruto anayewania kwa tikiti ya Chama cha Mashinani (CCM).

Ndoto ya Mbunge wa Kajiado Mashariki, Peris Tobiko ya kupeperusha bendera ya UDA katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kajiado ilikosa kutimia baada ya kushindwa na Mbunge wa Kajiado Kusini, Katoo Ole Matito.

Bi Tobiko alitisha kuwania kiti hicho kama mwaniaji wa kujitegemea akidai shughuli hiyo ilizongwa na visa vingi vya udanganyifu.

Katika kaunti ya Tharaka Nithi, azma ya Mbunge wa Mwakilishi wa Kike Beatrice Nkatha ya kutetea wadhifa huo kwa tiketi ya UDA ilikosa kutimia aliposhindwa na Bi Beatrice Kathomi.

Bi Kathomi ambaye ni mwanasiasa chipukizi alizoa jumla ya kura 49,327 dhidi ya kura 23,860 za Bi Nkatha kulingana na matokeo yaliyotangazwa jana alasiri.

Na Vitalis Kimutai, Alex Njeru, Stanley Kimuge, Eric Matara, Onyango K’Onyango, Tom Matoke

 

  • Tags

You can share this post!

Fortune yapania kusajili watatu

Serikali yaongeza muda wa kusajili laini za simu hadi...

T L