• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 8:50 AM
Mkono wa Rais Ruto ulivyomtoa Wamatangi vinywani mwa MCAs

Mkono wa Rais Ruto ulivyomtoa Wamatangi vinywani mwa MCAs

NA SIMON CIURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua, kwa mara ya pili katika muda wa chini ya miezi minane ameitisha mkutano na viongozi waliochaguliwa Kiambu.

Bw Gachagua anataka kuepusha hatua ya kumtimua Gavana Kimani Wamatangi ambaye ametofautiana waziwazi na wawakilishi wengi wa wadi, seneta wa eneo na wabunge wa kaunti hiyo.

Taifa Leo imebaini kuwa Bw Wamatangi aliwasiliana na Bw Gachagua kibinafsi kufuatia kubainika kuwa wazo la kuwasilishwa kwa hoja ya kutimuliwa kwake katika bunge la kaunti lilikuwa ukingoni na linazidi kushika kasi baada ya kuingia kwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah ambaye pia ni Mbunge wa Kikuyu na mshirika wa karibu wa Rais William Ruto.

Naibu Rais, alifahamu kuhusu mipango ya kumng’atua baada ya taarifa kutoka kwa Wamatangi kumfikia Rais Ruto ambaye alimtuma naibu wake kuokoa hali hiyo kwa masharti magumu kwamba lazima Gavana Wamatangi atimize matakwa ya wawakilishi wa wadi.

Viongozi wa kaunti hiyo wanamshutumu Bw Wamatangi kwa unyonge na utoaji wa huduma polepole haswa katika idara ya afya na barabara.

Isitoshe, anashtumiwa kwa kuwa na dosari katika ugawaji wa basari na kutohusisha wawakilishi wa wadi hata kwa miradi ambayo ilikuwa chini ya mamlaka yao.

Mzozo mwingine ni kuhusu bima ya matibabu yenye utata ya Sh319 milioni ambayo wawakilishi wa wadi wanadai ilitolewa na kampuni ya bima ya Mauritius ya MUA Insurance Limited.

Gavana Wamatangi ameendelea kupinga madai hayo, akisisitiza kuwa ni zabuni ya wazi ambayo ilitangazwa kwenye vyombo vikuu vya habari.

Mkutano wa Jumatatu, uliofanyika katika Makao Rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen uliohudhuriwa na viongozi wote waliochaguliwa Kiambu, ulifichua mzozo kati ya Wamatangi na wawakilishi wengi wa wadi katika Kaunti ya Kiambu ambapo mbele ya Naibu Rais Gachagua, Gavana Wamatangi aliazimia kuanzisha Hazina ya Maendeleo ya wadi ya Sh600 milioni.

Mkutano huo, kwa mujibu wa wadadisi wa mambo katika afisi ya Naibu Rais waliozungumza na Taifa Leo mnamo Jumatano, ulichukua muda wa saa nane.

“Naibu Rais alisikiliza MCAs 86, Wabunge wa Bunge la Kitaifa kutoka kaunti, seneta na gavana kando kabla ya kuitisha mkutano wa pamoja ambapo uamuzi ulitangazwa,” taarifa kutoka afisi ya Naibu Rais iliyoonekana na Taifa Leo inasema.

“Sina shida kuanzisha Hazina ya Maendeleo ya Wadi katika Kaunti ya Kiambu. Tutaitekeleza mara moja, pamoja na Bunge (Bunge la Kaunti). Tutawapa madiwani fursa ya kuchagua miradi ya kupatiwa kipaumbele. Hii itakuwa Sh10 milioni kwa kila wadi, ambapo wadi zetu 60 zitatumia jumla ya Sh600 milioni kati ya bajeti ya maendeleo ya Sh2.8 bilioni,” Bw Wamatangi alinukuliwa akisema.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Mwangaza alivyoangusha kibomu cha video kilichofanya...

Hofu genge la uhalifu likilenga sasa kupora wamiliki wa...

T L