• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Jinsi Mwangaza alivyoangusha kibomu cha video kilichofanya maseneta kuingia upande wake

Jinsi Mwangaza alivyoangusha kibomu cha video kilichofanya maseneta kuingia upande wake

NA MARY WANGARI

GAVANA wa Kaunti ya Meru Kawira Mwangaza mnamo Jumatano alikabiliwa na wakati mgumu akijitetea mbele ya Seneti kuhusiana na malalamishi yaliyowasilishwa dhidi yake na Bunge la Kaunti ya Meru.

Hali ya suitafahamu iligubika Bunge la Seneti baada ya video zilizokusudiwa kutumiwa na kikosi cha mawakili tisa wanaomwakilisha Gavana Kawira, kukumbwa na hitilafu za sauti mwanzoni na kuchelewesha kikao hicho, kilichoingia siku ya pili, kwa karibu saa moja.

Ilimlazimu Spika wa Seneti Amason Kingi kuingilia kati na kuwaagiza mafundi wa mitambo kumaliza mushkili huo uliotishia kuvuruga ushahidi wa mmoja kati ya mashahidi wanne wa Bi Kawira.

Gavana huyo alitokwa na kijasho huku mawakili wawili wanaowakilisha Bunge la Kaunti ya Meru wakimtaka kufafanua kuhusu madai ya usimamizi mbaya na ufujaji wa pesa za umma, yakiwemo matumizi mabaya ya afisi, kwa kuruhusu jamaa zake kusimamia majukumu ya fedha za kaunti.

Kuhusu kauli ya kaende kaende, gavana huyo alikanusha kuwa ilidhamiriwa kuonyesha ukaidi akifafanua kwamba ilimaanisha kuashiria kasi ya kutekeleza ajenda yake ya maendeleo katika Kaunti ya Meru.

“Nilitumia kauli ya kaende kaende kabati kabati kwa sababu inaashiria maendeleo. Inamaanisha kuendeleza maendeleo kwa kasi ya juu bila kukatiza,” alifafanua.

Kupitia wakili wake Elisha Ongoya, Bi Kawira alipuuzilia mbali madai ya kumtusi na kumdhalilisha naibu gavana wake Isaac Mutuma kwa kutumia maafisa wa ngazi za chini na makundi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Gavana huyo alieleza kuwa si yeye aliyekuwa akiendesha makundi hayo wala hajui jinsi alivyojiunga nayo wala aliyemjumuisha.

Aidha, alionekana kumlaumu naibu wake kupitia video iliyomwonyesha Bw Mutuma akiimba nyimbo za kumpinga yeye akiwa na kundi la watu wengine.

Katika mojawapo ya video, Mbunge wa Tigania Mashariki Mpuru Aburi anaonekana akitumia maneno machafu na kile kilichofasiriwa kwenye Seneti kuwa vitisho vya dhuluma za kijinsia dhidi ya Bi Mwangaza.

Aidha, Gavana Kawira alifafanua kuhusu ziara ya China iliyowajumuisha jamaa zake wanne badala ya maafisa wa afya wa Meru kuhusiana na Kituo cha Matibabu ya Saratani. Kulingana na Bi Kawira, alilazimika kuvunja safari ya kwenda China baada ya kugundua kampuni iliyokuwa imezuru afisi yake ilikuwa kundi la watu waliotaka kufanya biashara na Kaunti ya Meru wala si kutoa ufadhili wa vifaa vya matibabu jinsi walivyoeleza awali.

“Kampuni hiyo kwanza ilijihusisha na serikali ya China. Kama kawaida nilituma kikosi changu kilichojumuisha msaidizi wangu, mlinzi na waziri wa afya kwa maandalizi. Lakini walipofika waligundua kampuni hiyo hata haina afisi China. Sikuona haja ya kusafiri na kupoteza wakati kwa ziara kama hiyo,” akajitetea.

Diwani wa Nyaki Mashariki, Josphat Kinyua aliyekuwa mmojawapo wa mashahidi wa Bi Kawira, alieleza Seneti jinsi Naibu Gavana alivyotumia vishawishi kuwavutia madiwani kuunga mkono hoja ya kumng’oa mamlakani Gavana wa Meru.

Shahidi huyo alisimulia jinsi hafla iliyokusudiwa kupanda miti ilivyogeuzwa ghafla hafla ya wazee wa Njuri Ncheke kuwalisha kiapo madiwani wa Meru ili waunge mkono hoja ya kumfurusha Bi Kawira.

“Hafla iliyopangiwa kupanda miti iligeuzwa tambiko la kula kiapo lililofanyika kwenye jukwaa la Meru. Madiwani wapatao 40 walialikwa na wazee wa Njuri Ncheke kula kiapo,” alieleza Kinyua.

Akaongeza: “Mzee mmoja wa Njuri Ncheke alisikika akiwaonya madiwani kuhusu adhabu kali na laana endapo wangeghairi baada ya kula kiapo.”

Kikao cha Jumatano kilichukua muda mrefu hadi saa ikabadilika na Alhamisi kuingia.

Mnamo saa sita na dakika chache usiku huo wa kuamkia Alhamisi, spika Kingi aliwaongoza maseneta kupiga kura, Bunge la Seneti likishindwa kumng’oa ofisini.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Jumanne iliamuliwa baada ya maseneta kusikiliza ushahidi wa madiwani na kumpa nafasi Gavana Mwangaza kujitetea. 

Spika Kingi alifafanua kabla ya shughuli ya upigaji kura, akisema maseneta wangepiga kura kwa kila mojawapo ya mashtata dhidi ya Gavana Mwangaza. Maseneta walipiga kura mara saba.

Shtaka la kwanza lilikuwa ni ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za kaunti. Maseneta 19 walipiga kura ya kukubaliana na madiwani huku maseneta 28 wakipiga kura ya ‘La’.

Shtaka la pili lilikuwa upendeleo wa jamaa na ukiukaji mwingine wa maadili. Maseneta watano waliunga mkono ang’olewe huku 42 wakipinga.

Katika shtaka la tatu la kuwadhalilisha viongozi wengine kura ilipigwa ambapo matokeo yalikuwa kwamba watatu walikubaliana na madiwani wa Meru huku 44 wakipinga.

Kwenye shtaka la nne, Gavana Mwangaza alimulikwa na madiwani kwa kufanya uteuzi unaokiuka mchakato unaohitajika ambapo katika upigaji kura, maseneta 20 wamekubaliana na madai hayo huku 27 wakipinga.

Nalo shtaka la tano likihusu kuidharau mahakama ambapo maseneta watatu wamekubaliana na madiwani lakini wakalemewa na 44 waliopinga.

Aidha kiongozi huyo wa Kaunti ya Meru alikabiliwa na shtaka la sita la kuipa barabara jina la mume wake Bw Murega Baichu. Maseneta wanne wamepiga kura ya ‘Ndiyo’ ambapo tena walilemewa na 43 waliopinga.

Shtaka la saba na la mwisho lilisema Gavana Mwangaza alidharau Bunge la Kaunti. Shtaka hilo limepata uungwaji mkono kutoka kwa maseneta 10 pekee, tena wakilemewa na 37 waliopinga.

“Seneti haijathibitisha kosa lolote hivyo Gavana Kawira Mwangaza anaendelea kuongoza Kaunti ya Meru,” amesema spika Kingi.

Ikiwa maseneta wangepitisha hata shtaka moja tu, basi Gavana Mwangaza angebanduliwa ofisini.

Sasa cha kusubiriwa ni kuona namna atakavyojinyanyua tena na kutafuta njia ya kushirikiana na madiwani waliopitisha hoja ya kumbandua.

Hii imekuwa mara ya pili kwa kesi dhidi ya Gavana Mwangaza kuwasilishwa na kujadiliwa katika Bunge la Seneti.

  • Tags

You can share this post!

Utafunaji miraa na michanganyiko ya ‘chewing gum’...

Mkono wa Rais Ruto ulivyomtoa Wamatangi vinywani mwa MCAs

T L