• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Hofu genge la uhalifu likilenga sasa kupora wamiliki wa maduka

Hofu genge la uhalifu likilenga sasa kupora wamiliki wa maduka

NA FARHIYA HUSSEIN

GENGE la wahalifu wenye visu na panga limeanza kulenga maduka ya Mombasa na kuwaibia wamiliki.

Wakiwa wamejihami kwa silaha hatari, wahalifu hao katika Kaunti ya Mombasa wamelemaza na kuwaua wengi, na kusababisha wasiwasi miongoni mwa wakazi.

Kuibuka tena kwa magenge ya watu wanaotumia panga kumezua hofu Mombasa huku eneo la Kisauni likiathirika zaidi.

“Wanazidi kuwa na nguvu, siku hizi wanafanya mashambulio yao mchana. Tunapoteza pesa nyingi kwa magenge ya wahalifu. Kuendesha biashara katika eneo la Bamburi kumekuwa gharama kwa upande wetu kama wafanyabiashara,” alisema Bw Ali Omar, mmiliki wa duka.

Wenye maduka walibaini visa vya uvamizi wa kiholela vimewalazimu kujizatiti kwa silaha kama vile visu na panga.

Licha ya kuwepo kwa kamera za CCTV katika maeneo mbalimbali ya kibiashara Kisauni, wenyeji walisema magenge hayo ya wahalifu bado huendeleza operesheni zao.

“Inasikitisha kuona watu wanalazimika kujihami ili kulinda biashara na maisha yao. Natumai mamlaka husika inaweza kuchukua hatua madhubuti kushughulikia suala hilo na kuhakikisha usalama wa jamii,” alisema Bw Abdallah Qali.

Mmoja wa waathiriwa wa mashambuliohayo, Bw Antony Macharia, alisema ilimbidi kusihi wanachama wa magenge hayo wasimdhuru walipomshambulia.

“Nakumbuka siku hiyo, ilikuwa mchana nikiwa naelekea nyumbani ambapo watu watano walinivamia, wengine wakiniibia huku wengine wakinijeruhi kwa panga walizokuwa wamebeba. Niliwapa kila kitu lakini bado waliishia kunipiga,” alisema Bw Macharia.

Klipu ya video ambayo wanaume watano wanaonekana wakishambulia duka moja imezua gumzo mtandaoni huku watu wakieleza wasiwasi kuhusu kuibuka upya kwa magenge ya wahalifu.

Wakazi na wafanyabiashara sasa wameitaka serikali kuingilia kati kabla hali haijawa mbaya zaidi.

“Watoto wetu wako nyumbani kwa likizo ndefu ya miezi miwili, hii ndiyo hali tunayotaka kujipata? Hili ni jambo kubwa mno na masuala ya ukosefu wa usalama yanapaswa kupewa kipaumbele,” alionya Bi Maimuna Naima, mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Mwenyekiti wa Ulinzi Shirikishi katika eneo la Mwandoni, Bw Gulama Abdulhussein, alitaja ukosefu wa ajira kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya vijana hao kujiunga na magenge ya uhalifu.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Kisauni, Bw Jamleck Mbuba, doria za polisi huendeshwa mchana na usiku ili kusaidia kudhibiti visa hivyo.

Bw Mbuba aliwataka waathiriwa wa mashambulio hayo kuripoti visa hivyo katika vituo vya polisi.

  • Tags

You can share this post!

Mkono wa Rais Ruto ulivyomtoa Wamatangi vinywani mwa MCAs

GWIJI WA WIKI: Abel Nyamari

T L