• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 6:55 AM
Mshindi wa kiti cha urais Dkt William Ruto atoa hotuba iliyosheheni ujumbe wa amani na matumaini

Mshindi wa kiti cha urais Dkt William Ruto atoa hotuba iliyosheheni ujumbe wa amani na matumaini

NA SAMMY WAWERU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatatu imemtangaza Dkt William Ruto kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Dkt Ruto amezoa kura 7,176,141 kiwango ambacho IEBC imesema kinawakilisha asilimia 50.49 ya kura zilizopigwa.

Ruto aliwania wadhifa hiuo pamoja na mgombea mwenza, Rigathi Gachagua kupitia tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

“Mimi Wafula Chebukati, mwenyekiti wa IEBC ninatangaza rasmi Ruto William Samoei, nambari ya kitambulisho: 6847208, amechaguliwa kihalali kama rais wa Jamhuri ya Kenya,” amesema Bw Chebukati, wakati akitoa tangazo hilo katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Kinara wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, amekuwa wa pili katika kinyang’anyiro hicho cha urais, akipata kura 6, 942, 930, idadi hii ikiwakilisha asilimia 48.85.

Kulingana na IEBC, idadi ya walioshiriki kupiga kura ni 14,164,561.

Bw George Wajackoyah wa Roots Party amezoa kura 61, 969 naye David Mwaure (Agano Party) 31, 989.

Chebukati alitangaza mshindi licha ya mgawanyiko kushuhudiwa katika IEBC, ambapo makamishna wanne walisema hawatajihusisha na matokeo hayo.

Makamishna hao hata hivyo walisema shughuli nzima ya uchaguzi haikuwa na dosari, hadi kipindi cha mwisho ambapo tofauti ziliibuka.

Hali ya vuta nikuvute ilishuhudiwa Bomas of Kenya, kabla ya Bw Chebukati kutangaza matokeo.

Baada ya kutangazwa mshindi na kopokezwa cheti, Dkt Ruto alitoa hotuba fupi.

Ameanza kwa kumpongeza Chebukati akimrejelea kama mtu mtulivu lakini asiyependa masihara.

“Uliwawekea watu wote matokeo katika tovuti ya IEBC ili wenyewe wajionee kwamba hakuna hila yoyote,”

Rais mteule amewapongeza viongozi wa kidini kwa kuelekeza taifa kwa njia iliyonyooka.

Ameahidi kushirikiana na viongozi wote waliochaguliwa na walio katika upinzani ili kuimarisha utoaji huduma nchini.

Amempongeza Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.

“Ninanuia kuendeleza miradi tuliyoanza na kuimarisha rekodi ya maendeleo ya utawala wa Rais Kenyatta ambaye amekuwa mkubwa wangu kwa miaka 10,” amesema Ruto.

Vilevile ameahidi kwamba hana moyo wa kulipiza kisasi dhidi ya baadhi ya viongozi na maafisa serikalini waliohangaisha mrengo wake wa Kenya Kwanza.

Mchana, ajenti mkuu wa Bw Raila, Saitabao ole Kanchory ambaye alikuwa ameandamana na baadhi ya wandani wa waziri mkuu huyo wa zamani, nje ya Bomas alisema wanatilia shaka matokeo yaliyotangazwa baadaye.

  • Tags

You can share this post!

Kipengele 141 cha Katiba: Kuapishwa kwa mshindi wa kiti cha...

Wingu jeusi lakumba mustakabali wa kisiasa wa Mudavadi...

T L