• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:46 AM
Mswada wa Fedha: Mikakati ya Azimio kuuzima imeiva

Mswada wa Fedha: Mikakati ya Azimio kuuzima imeiva

Na BENSON MATHEKA

MUUNGANO wa Azimio La Umoja-One Kenya, unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, tayari umeweka mikakati ya kupinga utekelezaji wa Mswada tata wa Fedha wa 2023 iwapo utapitishwa bungeni.

Haya yanajiri huku upande wa serikali ukionyesha nia ya kulegeza msimamo kwa kuashiria utakubali kufanyia mabadiliko mswada huo.

Kulingana na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi, Azimio imejiandaa kuhakikisha mswada huo hautatekelezwa ukipitishwa kwa kuupinga kortini.

“Hatujapungukiwa na mbinu, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha kesi mahakamani. Pia tuna hatua nyingi. Huu ndio wakati ambapo maandamano yatafaa zaidi kuliko wakati mwingine wowote,” mbunge huyo aliambia wanahabari Jumanne.

Bw Wandayi alidokeza kuwa hatua yao ya kupinga Mswada huo kwa ujumla wake, ilitokana na Ruto kuwatishia wabunge wanaoegemea upande wake wakikataa Mswada huo Bungeni akisema rais hana mamlaka ya kuwaelekeza wabunge jinsi ya kupigia kura Mswada wowote.

“Kwa mujibu wa Katiba mpya, hakuna mtu nje ya Bunge anayeweza kuwaelekeza wabunge wapige kura kwa njia fulani, amepotoshwa. Maagizo yake yoyote yanaweza tu kupokelewa kupitia wawakilishi wa chama chake, akiwemo Kiongozi wa Wengi (Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah),” alisema.

Hata hivyo, Wandayi hakueleza ni lini wataenda kortini au kurudia maandamano.

Mjadala kuhusu Mswada wa Fedha 2023 unatarajiwa kuanza Alhamisi, Juni 8, wiki moja kabla ya Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u kusoma Bajeti ya 2023/24 Alhamisi, Juni 15.

Iwapo Azimio itaenda kortini, Ruto atakabiliwa na kesi mbili kwa kuwa Seneta wa Busia Okiya Omtatah amewasilisha kesi dhidi ya Mswada huo.

Omtatah anataka kumzuia Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, kuuwasilisha kwa Rais autie saini kuwa sheria iwapo wabunge wataupitisha.

  • Tags

You can share this post!

‘Shetani’ aingia kanisani na kutawanya na kujeruhi...

Waziri Soipan Tuya apongezwa kwa kuomba kwa Kiswahili...

T L