• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Mudavadi akataa kumezwa na UDA

Mudavadi akataa kumezwa na UDA

NA KALUME KAZUNGU

VINARA wa Chama cha Amani National Congress (ANC), kinachoongozwa na Mkuu wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, wamepinga shinikizo za chama cha UDA kuwa vyama tanzu vya Kenya Kwanza vivunjiliwe mbali.

Katibu Mkuu wa UDA, Bw Cleophas Malala amekuwa akiongoza mchakato wa kuvishawishi vyama vyote vya Kenya Kwanza kuvunjiliwa mbali na kuunda chama kimoja cha UDA, tangu alipohamia chama hicho rasmi wiki iliyopita.

Bw Malala pia aliwatishia vinara wa vyama tanzu waliopewa nyadhifa kubwa serikalini kwamba watazipoteza iwapo watakataa kuvunja vyama vyao.

Wakuu wa Bodi ya Maamuzi ya ANC waliokutana kisiwani Lamu jana Jumapili, walisema mkataba wao katika Kenya Kwanza haukuwa na sehemu yoyote kwamba vyama vitatakikana kuvunjwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Kiongozi wa chama hicho, Bw Issa Timamy, ambaye pia ni gavana wa Lamu, akiandamana na Mwakilishi wa Kike wa Vihiga, Bi Beatrice Adagala (Kaimu Katibu Mkuu), Mwenyekiti wa chama, Bw Kelvin Lunani na wengineo, walisema hawataunga mkono juhudi za kuvuruga demokrasia kwa kuondoa siasa za vyama vingi.

Bw Timamy alisema kuvunja vyama na kuunda UDA ni sawa na kuirudisha Kenya hadi mfumo wa zamani wa chama kimoja cha kisiasa ambao Wakenya waliukataa zamani.

Alisema Kenya ina matatizo ya kimsingi ikiwemo hali duni ya kiuchumi, gharama ya juu ya maisha, bei ghali ya chakula, usalama na ukame, ambayo yanafaa kupewa umuhimu badala ya siasa za vyama.

“Sisi kama ANC hatutakubali kuvunja chama chetu. Tutaendelea kuheshimu na kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza kama chama tanzu. ANC ni chama kinachojisimamia na ni vyema mjadala wa kuvunjilia mbali vyama, ambao unalenga uchaguzi wa 2027, kutupiliwa mbali na kuelekeza juhudi zetu katika kuhudumia wananchi,” akasema Bw Timamy.

Katika mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la Sunday Nation, Bw Malala alisema lengo la UDA ni kuhakikisha vyama vyote tanzu vimevunjwa kufikia Agosti ili uchaguzi wa viongozi wapya uandaliwe.

Kulingana naye, Kenya Kwanza iliundwa si kwa lengo la kupata mamlaka pekee bali kutatua changamoto zinazokumba nchi.

“Lengo letu kama chama kimoja litakuwa ni kuleta pamoja mawazo yetu ili tutatue changamoto hizo mara moja,” akasema.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, vinara wa vyama tanzu watakuwa hatarini kupoteza ushawishi wao mbele ya Rais William Ruto, aliye kiongozi wa UDA iwapo watakubali kuvunja vyama.

Mbali na Bw Mudavadi, vinara wengine ambao huenda wakaathirika kiushawishi ni Spika wa Bunge, Bw Moses Wetang’ula wa Chama cha Ford Kenya, Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi (Pamoja African Alliance), Mwanasheria Mkuu, Bw Justin Muturi (DP), na Waziri wa Kigeni, Dkt Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap).

Vinara hao walipewa nyadhifa kubwakubwa serikalini kwa msingi wa ushawishi waliodhihirisha katika ngome zao za kisiasa kupitia kwa vyama vyao.

Hivi majuzi, ilifichuka kuwa Dkt Mutua alipunguziwa mamlaka katika wizara yake ingawa serikali ilidai hatua hiyo inalenga kuboresha uwezo wa nchi za kigeni zinaposhirikiana na idara mbalimbali za humu nchini moja kwa moja.

Bi Adagala alidai Bw Malala ni ajenti wa mrengo wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya ambaye lengo lake ni kugawanya Kenya Kwanza kwa kuwachanganya watu na “kuwaacha kwenye mataa” ili kuwapa wapinzani nafasi.

Kulingana naye, ajenda kuu ambazo Wakenya wanahitaji kusikia ni jinsi uchumi utakavyoimarishwa na maisha yao kuboreshwa.

“Tulikuwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu miezi sita pekee iliyopita. Kwa sasa Wakenya wanachotarajia ni viongozi waliowachagua kuwahudumia wala si kuwarudisha kwenye kampeni nyingine kuhusu vyama. Wanaozunguka wakipiga kelele kuhusu vyama kuvunjiliwa mbali na kuunda chama kimoja cha UDA ni wale ambao wanafanyia kazi mrengo wa Azimio la Umoja kisiri,” akasema Bi Adagala.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni iliyofilisi raia ililindwa na polisi na wanasiasa...

Sh75m za ruzuku ya mafuta zilipotea kila siku – Ripoti

T L