• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:55 AM
Mudavadi ayumba uchaguzi ukibisha

Mudavadi ayumba uchaguzi ukibisha

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi anaendelea kuwakanganya wafuasi wake kwa kukosa msimamo thabiti huku Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 ukikaribia.

Bw Mudavadi pia anaonekana kuyumbayumba ndani ya One Kenya Alliance (OKA), hali ambayo inatishia uthabiti wa muungano huo.

Hii imewaacha wafuasi wa Bw Mudavadi bila uhakika ikiwa ataunga mkono Naibu wa Rais William Ruto au kinara wa ODM Raila Odinga au atawania urais.

Ikiwa ataamua kuwania urais, haijulikani ikiwa atatumia chama chake cha ANC au atapeperusha bendera ya OKA.

Wadadisi wanasema kuwa kutapatapa huko ni ishara kwamba Bw Mudavadi hajajipanga kisiasa.

“Tangu uchaguzi wa 2017, Bw Mudavadi hajaonyesha bidii kwamba anataka kuwa rais. Mara amekuwa akiunga mkono ama kukosoa serikali kwa wakati mmoj. Hajakuwa na msimamo thabiti,” anasema Bw Javas Bigambo, wakili na mtaalamu wa masuala ya utawala.

Mpasuko ndani ya OKA ulijitokeza wazi wikendi ambapo Bw Mudavadi alitoa ratiba ya kukinzana na ratiba iliyotolewa na makao makuu ya muungano huo.

Bw Mudavadi Jumapili alihudhuria ibada katika Kanisa la Redeemed Gospel lililoko kwenye Barabara ya Likoni jijini Nairobi. Baadaye mchana alienda kushuhudia mechi baina ya AFC Leopards na Nzoia Sugar FC uwanjani Nyayo.

Bw Mudavadi alikuwa ameandamana na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo.

Lakini mwaliko uliotumwa kwa vyombo vya habari Jumamosi na OKA ulionyesha kuwa vigogo wa muungano huo – Bw Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Bw Cyrus Jirongo (UDP), walifaa kuhudhuria ibada katika kanisa la Ziwani AIC, Nairobi.

Baadaye, Bw Mudavadi alijitetea kuwa alikosa kuandamana na vinara wenzake katika Kaunti ya Kajiado kutokana na matatizo ya kiafya.

Wadadisi wanasema kuwa kutapatapa kwa Bw Mudavadi kuhusiana na Mswada wa Marekebisho wa Vyama vya Kisiasa 2021 uliopitishwa na Bunge la Kitaifa Januari 4, mwaka huu, pia kuliashiria kwamba amekosa msimamo.

Awali, Bw Mudavadi alikuwa amepinga mswada huo lakini baadaye alibadili nia na kusema kwamba ulikuwa muhimu katika kuimarisha miungano ya kisiasa.

Wabunge wa ANC wakiongozwa na mbunge wa Lugari Ayub Savula walikuwa wameshikilia kwamba mswada huo ulikuwa mtego wa kushinikiza vinara wa OKA kuunga mkono Bw Odinga au Naibu wa Rais Ruto.

Mswada huo unaanza kushughulikiwa katika Seneti leo huku macho ya Wakenya yakielekezwa kwa maseneta wawili wa ANC, Bw Cleophas Malala (Kakamega) na Bw Khaniri George (Vihiga).

Bw Malala anaonekana kuegemea mrengo wa Dkt Ruto. Naibu wa Rais alikuwa mgeni wa heshima katika fainali za kombe la Cleo Malala Super Cup lililoandaliwa na Bw Malala mjini Mumias, Kaunti ya Kakamega mnamo Disemba 31, 2021.

Chama cha ANC kilijitenga na Bw Malala kupitia taarifa iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii.

Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Bw Mudavadi kukosa kumkaripia Bw Malala inafanya Wakenya kuamini kwamba madai yanayotolewa na seneta huyo wa Kakamega yana ukweli.

Bw Bigambo anasema kuwa iwapo Bw Mudavadi ataungana na Dkt Ruto, watampokonya Bw Odinga kiasi fulani cha kura katika eneo la Magharibi.

You can share this post!

Simiyu afurahishwa na matayarisho ya Shujaa

Wafanyikazi wasitisha mgomo Mombasa baada ya kulipwa

T L