• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Muthama amteua Prof Muli kuwa mwaniaji mwenza

Muthama amteua Prof Muli kuwa mwaniaji mwenza

NA KENYA NEWS AGENCY

MWANIAJI wa ugavana wa Machakos kupitia tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama, amemteua mkurugenzi wa Chuo cha Utabibu cha Machakos (MTTC) Prof Faith Muli kuwa mgombea mwenza wake.

Akizungumza katika Shule ya Sekondari ya Kitulu ambapo alienda kufariji familia ya aliyekuwa mbunge wa Machakos Onesmus Kimuyu, Bw Muthama alisema kuwa Prof Muli ana uwezo wa kuhudumia vyema wakazi wa Machakos.

“Nilikuwa namsaka kiongozi mnyenyekevu anayesikiliza, kutangamana na kutatua changamoto zinazokumba wazee. Prof Muli ana sifa hizo zote,” akasema Bw Muthama.

Alisema kuwa mkuu huyo wa MTTC ‘hana ubaguzi na anatangamana na mtu yeyote bila kujali kiwango cha elimu wala mapato.

Bw Muthama ni mwaniaji wa pili wa ugavana wa Machakos kutangaza mwaniaji mwenza wake baada ya aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi katika Ikulu, Nzioka Waita, wa Chama cha Uzalendo (CCU).

Bw Waita aliteua Spika wa Bunge la Kaunti ya Machakos Florence Mwangangi kuwa mwaniaji mwenza wake.

Wengine wanaomezea mate ugavana wa Machakos ni aliyekuwa Waziri Msaidizi (CAS) wa Uchukuzi Wavinya Ndeti, mbunge wa Mavoko Patrick Makau na Naibu Gavana wa Machakos Francis Maliti. Wakili Kyatha Mbaluka anapigania useneta .

  • Tags

You can share this post!

Wanabiashara wa miraa wakashifu serikali kwa kukosa...

Ivory Coast wampiga kalamu kocha Patrice Beaumelle

T L