• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Ivory Coast wampiga kalamu kocha Patrice Beaumelle

Ivory Coast wampiga kalamu kocha Patrice Beaumelle

Na MASHIRIKA

SHIRIKISHO la Soka la Ivory Coast (FIF) limemtimua kocha Patrice Beaumelle baada ya mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 43 kushindwa kuongoza miamba hao kutoka Afrika Magharibi kusonga mbele zaidi ya hatua ya 16-bora kwenye fainali zilizopita za Kombe la Afrika (AFCON) 2021.

Ivory Coast ambao ni mabingwa mara mbili wa AFCON walidenguliwa na Misri kupitia penalti baada ya sare tasa kwenye 16-bora katika makala yaliyopita ya kivumbi hicho kilichofanyika nchini Cameroon. Baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo Novemba-Disemba 2022, Beaumelle ambaye ni raia wa Ufaransa alishutumu Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa “kuua soka ya Afrika” kwa kutengea bara la Afrika tiketi tano pekee katika kipute hicho cha haiba kubwa.

Beaumelle alikuwa msaidizi wa kocha Herve Renard Ivory Coast walipotawazwa wafalme wa AFCON mnamo 2015. Amekuwa akidhibiti mikoba ya miamba hao tangu Machi 2020. Amewahi pia kudhibiti mikoba ya Zambia baada ya kuwa msaidizi wa Renard kambini mwa kikosi hicho almaarufu Chipolopolo.

Ivory Coast watakaokuwa wenyeji wa fainali zijazo za AFCON 2023, ndicho kikosi cha hivi karibuni zaidi kuagana na mkufunzi wao huku Burkina Faso na Mali pia wakisaka makocha wapya.

You can share this post!

Muthama amteua Prof Muli kuwa mwaniaji mwenza

Uamuzi wa Haji kutowashtaki wanasiasa kwa ufisadi wazua joto

T L