• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Mutua, Kingi watafuta hifadhi kwa Ruto, wadai kuumizwa katika Azimio

Mutua, Kingi watafuta hifadhi kwa Ruto, wadai kuumizwa katika Azimio

NA WAANDISHI WETU

MAGAVANA Alfred Mutua wa Machakos na mwenzake wa Kilifi, Amason Kingi jana Jumatatu walihama muungano wa Azimio wakidai kunyanyaswa.

Gavana Kingi alisema alijiondoa Azimio kwa kile alieleza kuwa kutengwa kwa chama chake cha PAA katika meza ya maamuzi.

Msemaji wa PAA, Lucas Maitha alisema Azimio ilimtenga kiongozi wa chama chao.

“Tugundua kulikuwa na njama fiche ya kumaliza vyama vidogo. Tulikuja kugundua kuwa Azimio ni kuhusu ODM, Jubilee na Wiper,” alisema.

Bw Maitha alisema kwamba Kenya Kwanza ya Dkt Ruto iliwahakikishia mgao katika serikali ijayo.Dkt Mutua alitangaza kuwa hakuweza kuvumilia alichotaja kama “ukosefu wa uwazi katika Azimio”.

“Tumeshawishika kwamba timu bora ya kubadilisha Kenya ni Kenya Kwanza na kiongozi wa kubadilisha Kenya ni William Ruto,” alisema Dkt Mutua.

Alidai kwamba ana habari kwamba vyama vingine vitano vinapanga kujiondoa katika Azimio kwa sababu ya ukosefu wa uaminifu na kutengwa kwa maeneo kuwa ya baadhi ya vyama vikubwa.

Baadhi ya viongozi wa vyama tanzu vya Azimio ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa uwazi ni Amason Kingi wa chama cha Pan African Alliance (PAA) na Profesa Kivutha Kibwana wa Chama cha Muungano.

Kulingana na Msajili wa vyama vya kisiasa, Ann Nderitu, mkataba wa Azimio umefunga vyama tanzu hadi miezi mitatu baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, Dkt Mutua alidai kwamba chama chake hakijawahi kupata nakala za mkataba huo licha ya kukiri kuutia saini.

Katika Kaunti ya Mombasa, Bw Ruto amemnyakua aliyekuwa mgombea mwenza Bw Suleiman Shabhal, Bi Selina Maitha.

Kulingana na duru za kuaminika, Bi Maitha aliona amesalitiwa baada ya kuacha kazi ya serikali na kujiunga na siasa.

Alikuwa ameteuliwa na Bw Shahbal kuwa mgombea mwenza wake Mombasa lakini baadaye akajiondoa kumpisha Abdulswamad Nassir.

Bi Maitha, ni dadake aliyekuwa waziri maarufu marehemu Karisa Maitha.

Na katika kaunti ya Kilifi, Ruto amemnyakua spika wa bunge hilo Bw Jimmy Kahindi ambaye alikuwa anataka kugombea ugavana kupitia ODM akijiunga na Kenya Kwanza.

“Timu ya Kenya Kwanza, Mombasa imepata nguvu baada ya mgombea mwenza wa Bi Maitha na wajumbe wake wakuu kujiunga na muungano wetu ili tulete mabadiliko ya uongozi Mombasa,” alisema Dkt Ruto.

Inadaiwa, Bw Kahindi alikuwa anamshurutisha mgombea wa ugavana wa Kilifi, Gideon Mung’aro kumchagua kama mgombea mwenza.

Ripoti ya Benson Matheka, Winnie Atieno na Maureen Ongala

 

  • Tags

You can share this post!

Naibu Gavana ahofia ODM kupoteza ugavana Kaunti ya Kilifi

Alfred Mutua asema Kenya Kwanza nd’o mpango mzima

T L