• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Mvurya awazidi maarifa Joho na Kingi, Achani akichukua Kwale

Mvurya awazidi maarifa Joho na Kingi, Achani akichukua Kwale

NA SIAGO CECE

GAVANA wa Kaunti ya Kwale Bw Salim Mvurya, ameonyesha ubabe wake wa kisiasa baada ya kumrithisha kiti cha ugavana naibu wake, Bi Fatuma Achani.

Bw Mvurya ambaye ameemuunga mkono Bi Achani hadi akatwaa uongozi wa kaunti hiyo, pia ameonyesha ubabe wake kwa kupita katikati ya Gavana wa Mombasa Ali Joho na Bw Amason Kingi wa chama cha PAA.

Ikizingatiwa kuwa Bw Joho alikuwa akimuunga mkono mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya chama cha ODM, Prof Hamadi Boga, na Bw Kingi akimpigia debe mgombea wa PAA, Bw Lung’azi Chai, ni wazi kuwa Bw Mvurya aliwazidi ujanja.

Kinyang’anyiro hicho cha ugavana wa kaunti ya Kwale, kiliibua ushindani mkali kati ya magavana hao watatu wanaoondoka, kuonyesha atakayekifaa chama chake.

Bw Joho alifanya kampeni katika maeneo bunge yote manne ya Kwale kumtafutia ushindi Prof Boga ila juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Kwa upande wake kiongozi wa chama cha PAA Bw Kingi, alijitahidi kumpigia debe Bw Lung’azi licha ya wao kuwa katika mrengo wa Kenya Kwanza na Bw Mvurya.

Imebainika kuwa, Bw Mvurya, aliamua kubaki katika eneo la Kwale na kutojihusisha sana na siasa za kitaifa huku akizindua miradi na naibu wake na kuwaomba wakazi wampigie naibu wake kura.

Bi Achani alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 59,674 huku Prof Boga aliyekuwa wa pili katika kinyang’anyiro hicho kikali, akimfuata kwa kura 53,972.

Akizungumza baada ya kutuzwa cheti cha ushindi, Bi Achani alimshukuru Bw Mvurya kwa kumlea kisiasa ili aichukue nafasi yake.

Alieleza kuwa ndiye aliyejitolea kumuunga mkono mwanamke.

Ushindi huu kwa sasa unamuidhinisha Bw Mvurya kama kiongozi mwenye usemi mkubwa katika eneo la Pwani, nafasi ambayo Bw Joho amekuwa akiishikilia kwa kuwa na ushawishi juu ya wakazi wa eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Chebukati ahimizwa akaze mkono ili kumaliza taharuki

Nani kama Wakenya!

T L