• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Mwandani wa Ruto ‘asaliti’ vijana

Mwandani wa Ruto ‘asaliti’ vijana

Na SAMWEL OWINO

WAKATI ambapo Naibu Rais Dkt William Ruto amekuwa akijiuza kama atakayewainua vijana kwa kuwatengea nafasi za ajira akichaguliwa 2022, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kiambu Gathoni Wamuchomba, mwandani wake, ameshangaza wengi kwa kudhamini mswada wa kuwarejesha waliostaafu kazini.

Bi Wamuchomba ambaye alivukia mrengo wa ‘Hasla’ miezi michache iliyopita kutoka kwa kambi ya ‘handisheki’, amewasilisha mswada bungeni ambao unalenga kuwarejesha kazini watumishi wa umma waliostaafu kutoa huduma kwenye idara mbalimbali za serikali.

Kati ya wastaafu ambao watarejeshwa kazini panapohitajika ni walimu, maafisa wa usalama, madaktari na watumishi wengine wa umma wataalamu.

Lengo la mswada huo ni kuhakikisha kuwa waliostaafu wanasalia wamethaminiwa uzeeni kinyume na sasa ambapo baadhi yao wanaendelea kuteseka maishani.

“Waziri kwa kushauriana na Tume ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma (PSC), tume nyingine huru, mashirika ya serikali na Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC), itawapa ajira waliostaafu kutoa huduma spesheli kwa muda uliokubalika. Sekta ambazo huduma zao zitafaa zaidi ni afya, usalama wa kitaifa, elimu na nyingine ambazo waziri ataona zinafaa kuimarishwa. Mswada huu utahakikisha kuwa hali ya maisha ya wakongwe inaimarika kuliko jinsi ilivyo kwa sasa ambapo baadhi wamelemewa na makali ya maisha,” ikaongeza sehemu ya mswada huo.

Iwapo mswada huo ambao upo katika hatua za mwanzo utapitishwa na hatimaye kutiwa saini na Rais, basi Baraza la Kitaifa la Wakongwe litabuniwa na litahusika sana kuhakikisha maslahi yao yanatimizwa.

Pia wakongwe ambao hawatakuwa wamerejeshwa kwenye huduma zinazotolewa, watahudumiwa nyumbani na wataalamu wa serikali.

Hii inalenga kuhakikisha wanaishi maisha ya starehe wala hawatatiziki kupata huduma muhimu kama matibabu na hata vyakula.

Hata hivyo, wengi wameshangazwa na mswada huo wa Bi Wamuchomba, ikizingatiwa amekuwa kati ya wanaovumisha ajenda ya hasla inayorindimwa na kambi ya Dkt Ruto.

Wanasiasa wanaounga mkono Naibu Rais wamekuwa wakiwarai vijana wawapigie kura, Dkt Ruto mwenyewe akiahidi kuwaajiri vijana milioni nne na kuwainua kibiashara kupitia mpango utakaogharimu Sh100 bilioni.

Kulingana na takwimu kutoka kwa KNBS, vijana milioni 7.6 hawana ajira licha ya kuwa wamehitimu vyema kutoka vyuo na taasisi mbalimbali za masomo.

Kinaya ni kwamba mbunge wa Starehe Charles Njagua Kanyi, naye aliwasilisha hoja bungeni mnamo 2019, ambayo ilitaka umri wa kustaafu upunguzwe kutoka miaka 60 hadi 50 ili kubunia vijana nafasi za ajira.

Ingawa hoja ya Bw Kanyi ilipitishwa bungeni, lazima aibadilishe iwe mswada ili sheria irekebishwe ndipo umri wa kustaafu upunguzwe hadi miaka 50 iwapo Rais atatia saini mswada huo.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta naye ameshutumiwa kwa kuwateua wakongwe kama wakuu wa mashirika mbalimbali.

Kwa mfano, aliyekuwa mkuu wa jeshi Julius Karangi ni mwenyekiti wa NSSF huku Francis Muthaura, 72 akiwa mkuu wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA).

You can share this post!

Oparanya apanga kuachia serikali kuu ujenzi wa hospitali ya...

Kampuni za kusaga mahindi zasitisha shughuli zao

T L