• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Kampuni za kusaga mahindi zasitisha shughuli zao

Kampuni za kusaga mahindi zasitisha shughuli zao

Na BARNABAS BII

KAMPUNI za kusaga mahindi katika maeneo ya Magharibi na Kati mwa Kenya, zimelazimika kusitisha operesheni zao kufuatia ukosefu wa mahindi wakati ambapo Wakenya milioni 2.5 nao wanakabiliwa na njaa.

Hatua za kampuni hizo kusitisha operesheni pia zitachangia wengi kupoteza ajira wakati takwimu zinaonyesha idadi ya Wakenya wasiokuwa na kazi inazidi kuongezeka.

Tayari kampuni 10 ambazo husaga mahindi zimewatuma wafanyakazi wao kwa likizo ya lazima baada ya kusitisha shughuli zao kutokana na ukosefu wa mahindi ambao umechangiwa na mavuno ya chini.

Idadi ya magunia ya mahindi yaliyovunwa msimu uliopita ni milioni 44 hii ikiwa kiwango cha chini ikilinganishwa na milioni 42.1 msimu wa 2019.

“Kampuni nyingi za kusaga mahindi zimekosa mazao hayo kwa muda wa wiki mbili iliyopita. Bei ya mahindi nayo imepanda hadi Sh3,000 kwa kila gunia ya kilo 90 na wamiliki wa kampuni hizo wamesema watarejelea operesheni zao iwapo kutakuwa na mahindi ya kutosha ya kusaga,” akasema Mwenyekiti wa Muungano wa Wasagaji Mahindi (GBMA), Bw Kipngetich Mutai.

Aidha kampuni zilizoathirika zinapatikana Bungoma, Busia, Kisumu, Narok, Kajiado na nyingine nne eneo la Kati.

Ukosefu wa mahindi umechangia kupanda kwa bei ya unga na unatokana na mavuno yasiyoridhisha msimu uliopita na pia hatua ya baadhi ya wakulima kuyahodhi mahindi yao wakisubiri bei ipande zaidi.

“Afadhali kampuni kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa hasa Eldoret, Moi’s Bridge na Kitale bado zina mahindi ila kiasi walicho nacho hakiwezi kuwafikisha hata miezi miwili,” akasema Bw David Koskei ambaye anamiliki kampuni ya kusaga mahindi mjini Eldoret.

Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) nayo imepandisha bei ya gunia la kilo 90 ya mahindi hadi Sh2,700.

Hata hivyo, kuna ushindani mkali huku kampuni za kusaga mahindi nazo zikipandisha bei hiyo hadi Sh2,900 ili kuwashawishi wakulima wawauzie mahindi.

Wananchi nao wataanza kuumia huku bei ya unga wa mahindi ikipanda hadi Sh105 kutoka Sh100 kwenye maduka mbalimbali eneo la Mlima Kenya na bei hiyo huenda ikapanda zaidi.

“Hatatakuwa na jingine ila kupandisha bei ya unga nao wateja wetu watalazimika kugharimika zaidi kuhakikisha wanapata mlo wa ugali,” akasema Bw Edwin Mutai mmoja wa wamiliki wa maduka ya kuuza bidhaa mjini Eldoret.

Wizara ya Kilimo nayo imefichua kuwa Kenya ina mahindi ambayo inaweza kufikisha nchi hadi Machi mwakani.

Muungano wa Wasaga Nafaka (CMA) ambao una kampuni tano za kusaga unga-Momabasa, Unga, Pembe, Dolan na Kitui, nao umesema kuwa umesalia na magunia machache ya mahindi ya kuwafikisha tu miezi michache ijayo.

You can share this post!

Mwandani wa Ruto ‘asaliti’ vijana

Makahaba kuandamana Uingereza kuhusu mauaji ya Wanjiru

T L