• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Ni midume tupu katika muungano wa Ruto

Ni midume tupu katika muungano wa Ruto

BENSON MATHEKA Na JURGEN NAMBEKA

NAIBU RAIS William Ruto jana alitia saini mkataba wa ushirikiano na vyama 12 chini ya Muungano wa Kenya Kwanza huku suala la ukosefu wa usawa wa jinsia likiibuka.

Vyama vyote vinavyounga azima yake vinasimamiwa na wanaume ishara kwamba, maamuzi yote ya muungano wa Kenya Kwanza huenda yatakuwa yakifanywa na jinsia moja.Japo alisifu washirika wake akisema waliungana bila vitisho, kukosekana kwa mwanamke miongoni mwa vigogo hao huenda kukazua mdahalo.

“Kenya Kwanza ni muungano unaojumuisha vyama vinavyoungana kwa hiari tofauti na waliotishwa kuunga muungano ule mwingine,” akasema Dkt Ruto wakati vyama hivyo vilitia saini mkataba wa ushirikiano.

Vyama ambavyo vilitia saini mkataba wa ushirikiano na chama cha United Democratic Alliance cha Dkt Ruto ni Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Musalia Mudavadi, Ford Kenya kinachoongozwa na Moses Wetangula, Chama cha Mashinani cha aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto, Democratic Party cha Spika wa Bunge Justin Muturi na Farmers Party cha aliyekuwa katibu wa wizara Irungu Nyakera.

Vyama vingine vilivyotia saini mkataba huo wa kuunga azima ya urais ya Dkt Ruto ni The Service Party cha aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Chama cha Kazi kinachoongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, Umoja, Maendeleo ambacho kiongozi wake ni Gavana wa Embu Martin Wambora na Tujibebe Party cha aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo.

Viongozi wa vyama hivyo wataungana na wale wa Devolution Party of Kenya, Communist Party na Economice Freedom Party katika muungano wa Kenya Kwanza.

Taswira hii ni tofauti na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambao vyama viwili miongoni mwa 26 vinavyounga azima ya urais ya kiongozi wa ODM Raila Odinga vinaongozwa na wanawake.

Gavana wa Kitui Bi Ngilu anayeongoza chama cha Narc na aliyekuwa waziri Martha Karua anayeongoza Narc Kenya ni wanachama wa Baraza la Azimio linalotarajiwa kutoa maamuzi ya mwisho katika muungano huo.

Hata baada ya kutia saini mkataba huo, Dkt Ruto ameonekana kuepuka migogoro katika Kenya Kwanza kwa kuhakikisha atagombea urais kwa tikiti ya chama chake na UDA, tofauti na Bw Odinga anayegombea kwa tikiti cha Azimio la Umoja.

Hii itahakikisha kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto atatoka katika chama chake iwapo hatashawishika kukabidhi wadhifa huo mmoja wa washirika wake.

Wadhifa huo umezua mgogoro katika Azimio la Umoja ambao baadhi ya washirika wa Bw Odinga wanapiga miereka wakiumezea mate.

Tayari, chama cha Wiper kinachoongozwa na aliyekuwa Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka kimeongoza baadhi ya vyama kuandikia msajili wa vyama vya kisiasa kutaka usajili wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance usitishwe hadi suala la atakayekuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga litatuliwe miongoni mwa masuala mengine.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Azimio la Umoja Raphael Tuju, viongozi wa vyama husika watazungumza na watasuluhisha mivutano inayokumba muungano huo.

Chama cha Wiper kilidai uongozi wa mkataba wa kwanza wa Azimio la Umoja- One Kenya Alliance ulibadilishwa.

“Makubaliano tuliyowasilisha yaliondolewa, na vifungu vikabadilishwa bila ruhusa za wanachama husika wala walioutia saini,” ilisoma sehemu ya barua ya One Kenya Alliance kwa msajili wa vyama.

Jana, Dkt Ruto alisifu washirika wake katika Kenya Kwanza akisema waliungana kwa moyo wa uaminifu tofauti na Azimio ambao umetawaliwa na kutoaminiana.

  • Tags

You can share this post!

Otuoma anyakua tikiti ya ODM kwa ugavana Busia

Mwalimu wa madrasa Marsabit ahofia maisha yake

T L