• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Njomo na wabunge wengine wa zamani wa Jubilee waunga mkono mapinduzi chamani

Njomo na wabunge wengine wa zamani wa Jubilee waunga mkono mapinduzi chamani

Na CHARLES WASONGA

BAADHI ya wabunge wa zamani wa Jubilee wamesema wanaunga mkono utawala wa Rais William Ruto wakati huu ambapo kuna mgawanyiko katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Wakiongozwa na mbunge wa zamani wa Kiambu Jude Njomo walisema wamefikia uamuzi huo kwa manufaa ya wakazi wa maeneo bunge yao.

“Tungali wanachama halali wa chama cha Jubilee. Lakini tunatambua uamuzi ambao umechukuliwa na kamati kuu ya kitaifa ya chama (NEC),” Njomo akawaambia wanahabari Jumanne.

“Tunaongeza kuwa hatutashiriki katika mambo yoyote ambayo yanalenga kuvuruga umoja na uwiano nchini,” akaongeza.

Bw Njomo pia ameaunga mkono uamuzi wa baraza la NEC la Jubilee la kuanza mchakato wa kujiondoa kutoka muungano wa Azimio ndani ya miezi sita ijayo.

Mbunge huyo alisema hayo alipokuwa ameandamana na wabunge wa zamani Maoka Maore (Igembe Kaskazini) na Mercy Gakuya (Kasarani).

Chama cha Jubilee ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio.

Mnamo Ijumaa Baraza la NEC la chama hicho lilikutana katika mkahawa mmoja mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru na kuamua kumsimamisha kazi Katiba Mkuu Jeremiah Kioni na Naibu Mwenyekiti David Murathe.

Aidha, mkutano huo ulioongozwa na mwenyekiti wa kitaifa Bw Nelson Dzuya na kuhudhuriwa na wabunge pamoja na maafisa wengine wa chama hicho kinachoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Chama hicho pia kiliamua kuondoka Azimio na kuanzisha ushirikiano na chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Rais Ruto ndio kiongozi wa kitaifa wa UDA alichokibuni baada ya kukosana na Bw Kenyatta katika muhula wa pili wa utawala wa Jubilee. Hii ni baada ya Bw Kenyatta kuamua kuridhiana kisiasa na aliyekuwa hasidi wake mkuu wa kisiasa Raila Odinga katika kile kilichojulikana kama “Handisheki”

Bw Kioni amepuuzilia mbali mapinduzi yaliyofanyika katika Jubilee huku akishikilia kuwa angali Katibu Mkuu halali.

  • Tags

You can share this post!

Shida ya pumu na jinsi unavyoweza kujihadhari nayo

Ruto akata miguu ya Raila bungeni

T L