• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
PAA sasa yamezwa na Kenya Kwanza, yashindwa kupaa

PAA sasa yamezwa na Kenya Kwanza, yashindwa kupaa

BRIAN OCHARO Na MAUREEN ONGALA

CHAMA cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kimeshindwa kuwika ndani ya muungano wa Kenya Kwanza kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Dalili zinaonyesha kuwa chama hicho kimemezwa na muungano huo kiasi cha kuwa wanachama wake hawana usemi tena katika mikutano ya hadhara ya muungano huo, ambayo hutumiwa kupigia debe wawaniaji wa viti mbalimbali Pwani kupitia chama cha UDA.

Katika ziara za Kenya Kwanza eneo la Pwani wikendi, wanachama wa PAA wakiongozwa na Bw Kingi hawakuonekana mikutanoni.

Bw Kingi alikuwa ameingizwa kwenye kamati ya viongozi wa Pwani wa kupanga mikakati ya Kenya Kwanza eneo la Pwani, akiwa pamoja na Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, na Mwakilishi wa Kike wa Taita Taveta, Bi Lydia Haika.

Jumapili, hakuhudhuria mikutano mitatu iliyoandiliwa katika kaunti yake ambayo iliongozwa na Dkt Ruto akiandamana na vinara wengine wakiwemo kinara wa Ford Kenya, Bw Moses Wetang’ula, mwezake wa ANC, Bw Musalia Mudavadi na kiongozi wa Maendeleo Chap Chap, Dkt Alfred Mutua.

“Bw Kingi hayuko nasi hapa kwa sababu amepatwa na shughuli,” Naibu Rais aliye kinara wa UDA aliwaambia waliohudhuria mkutano huo.

Kati ya wanasiasa wa Pwani waliokuwepo, waliokuwa mstari wa mbele kuhutubu walikuwa Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, na Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya ambao wote ni wafuasi wa UDA.

Bw Kingi alidai kuwa hakuhudhuria mikutano ya Kenya Kwanza eneo la Pwani kwa sababu anashughulikia mambo ya familia yake jijini Nairobi.

“Nimekuwa ninashughulikia mambo ya familia jijini Nairobi. Na sio Kenya Kwanza tu, nimekosa kuhudhuria mikutano ya PAA inayoendelea,” akasema.

Hata hivyo, huu si mkutano pekee wa Kenya Kwanza ambapo wawaniaji wa PAA hawajaonekana.

Wawaniaji viti kupitia kwa PAA na UDA eneo la Pwani wamekuwa wakiendeleza kampeni zao tofauti.

Bi Jumwa na Bw Baya huendeleza kampeni ya wilbaro sita kumaanisha wanataka wapigakura kuchagua wagombeaji wote wa UDA, huku Bw Kingi na wanachama wake wakipigia debe PAA Tano na wilbaro moja kumaanisha wagombeaji wote wa PAA wachaguliwe kuanzia diwani hadi gavana, na mgombeaji mmoja wa UDA ambaye ni Dkt Ruto kwa urais.

Idadi kubwa ya wagombeaji wa viti kupitia PAA wameonekana pia kuepuka kutumia nembo za Kenya Kwanza wala sura ya Dkt Ruto katika mabango yao ya kampeni.

Wadadisi wa kisiasa wanahoji kuwa, huenda uamuzi uliotolewa kwamba PAA na Maendeleo Chap Chap haziwezi kuingia Kenya Kwanza kwa kuwa zilikuwa tayari na mkataba katika Azimio la Umoja One Kenya, limekanganya wanachama wao.

“Wengi wao wamejipata wamemezwa na vyama vikubwa na hawana la kufanya,” akasema wakili Joseph Munyithia.

Bw Kingi na Dkt Mutua awali walikuwa katika Azimio, lakini wakaondoka baadaye wakidai kuna usiri mwingi katika muungano huo wa kinara wa ODM, Bw Raila Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Mdahalo: Wawaniaji ugavana wafafanulia wakazi wa Kiambu...

KINYANG’ANYIRO 2022: Kaunti ya Kisumu

T L