• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Polisi watibua maandamano ya Azimio IEBC

Polisi watibua maandamano ya Azimio IEBC

NA MARY WANGARI

MAAFISA wa polisi jana walikabiliana vikali na viongozi wa Azimio One Kenya waliokuwa wakiandamana kulalamikia hatua ya kumfuta kazi naibu mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ruth Kulundu.

Hali ya sintofahamu ilizuka baada ya walinda usalama kulazimika kurusha vitoa machozi ili kuwatawanya wanasiasa na wafuasi wa Azimio waliokuwa wakiandamana kuelekea kwenye afisi za IEBC katika jengo la Anniversary Towers, jijini Nairobi.

Hata hivyo, juhudi za wanasiasa hao wanaoegemea kambi ya Raila Odinga, za kukutana na viongozi wa IEBC, ziligonga mwamba huku afisi za Tume hiyo zikiwa chini ya ulinzi mkali kutoka kwa maafisa wa GSU waliojihami na malango yake kufungwa.

Wakihutubia wanahabari Jumatatu nje ya lango la afisi za IEBC, viongozi wa Azimio wakiongozwa na Mbunge wa Makadara George Aladwa, walitishia kuwachukulia hatua kali mwenyekiti na mkurugenzi wa IEBC, Wafula Chebukati na Marjan Hussein Marjan mtawalia, iwapo hawatamrejesha kazini mara moja Bi Kulundu.

“Kinachofanyika katika IEBC si sawa. Maafisa wa IEBC wameandikwa kwa pesa za wananchi. Na sisi kama walipa ushuru, tunasikitishwa kuwa kuna wale wanaotolewa kinyume na sheria,” alisema Bw Aladwa.

Aidha, waliipatia Tume ya Uchaguzi makataa ya saa 24 kumrejesha kazini Bi Kulundu la sivyo wachukue hatua ikiwemo kumshinikiza mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kujiuzulu.

“Matakwa yetu ni kuwa: IEBC imrejeshe kazini mara moja Bi Kulundu katika wadhifa wake wa naibu mkurugenzi katika muda wa saa 24 zijazo la sivyo tutawachukulia hatua kali Mwenyekiti Wafula Chebukati na Mkurugenzi Marjan Hussein Marjan,” ilisema taarifa kutoka kwa viongozi wa Azimio.

“IEBC imdhibiti Bw Marjan Hussein na iwaonyeshe Wakenya kuwa ataheshimu maadili na kanuni za utumishi wa umma la sivyo tutamshinikiza kujiuzulu kutoka kwa wadhifa wake kabla ya kuanza mchakato wa kufanyia marekebisho mipaka au kufanya chaguzi ndogo zilizosalia.”

Wanasiasa hao wameishutumu vikali Tume ya Uchaguzi kwa kile wanachotaja kama kuwalenga maafisa wanaochukuliwa kwamba wanaegemea kambi ya Azimio hasa kuhusiana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, ambapo Rais William Ruto aliibuka mshindi.

Kando na hatua ya kumfuta kazi Bi Kulundu, kambi ya Bw Odinga vilevile inawashutumu maafisa wakuu wa IEBC dhidi ya kuendeleza ubaguzi, kupendelea jamaa wa familia na sera za ajira zinazokiuka sheria.

Mbunge wa Embakasi Magharibi, Mark Mwenje alilalamikia hatua ya maafisa wa polisi ya kuwazuia viongozi wa Azimio kupata haki akisema IEBC imekiuka sheria za wafanyakazi.

“Hii ni afisi ya umma. Tuna haki ya kuingia. Hata baada ya kujitambulisha maafisa wa polisi walitukataza kuingia wakisema tumekuja na wahuni ilhali hatujavunja sheria yoyote. Wao ndio wamekiuka sheria ya waajiriwa,” alisema Bw Mwenje.

  • Tags

You can share this post!

Usambazaji wa chakula cha msaada waanza rasmi

SHINA LA UHAI: Maradhi yasiyosambaa yaendelea kuwa mzigo...

T L