• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 4:32 PM
SHINA LA UHAI: Maradhi yasiyosambaa yaendelea kuwa mzigo mzito

SHINA LA UHAI: Maradhi yasiyosambaa yaendelea kuwa mzigo mzito

NA PAULINE ONGAJI

MIONGONI mwa watu kumi wanaokufa, saba kati yao hufariki kutokana na maradhi yasiyosambaa.

Kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Duniani WHO, maradhi haya ambayo kwa Kiingereza yanafahamika kama non communicable diseases NCDs, yanasababisha zaidi ya asilimia 74 ya vifo duniani, na asilimia 80 ya vifo hivi ni kutoka mataifa yanayostawi, Kenya miongoni mwao.

Hapa nchini, maradhi yasiyosambaa yameonekana kuendelea kuongezeka na sasa yanasemekana kusababisha asilimia 46 ya vifo vyote nchini, huku walio chini ya umri wa miaka 40 wakionekana kuathirika pakubwa.

Isitoshe, asilimia 50 ya watu wanaolazwa hospitalini wanaugua maradhi haya huku asilimia 55 ya vifo hospitalini na asilimia 39 ya vifo vyote hapa nchini vikiwa kutokana na magonjwa haya.

Miaka miwili iliyopita, takwimu za Wizara ya Afya zilionyesha kwamba asilimia 39 ya vifo nchini vilitokana na maradhi yasiyosambaa. Ongezeko hili lilikuwa kutoka asilimia 27 mwaka wa 2014, huku ikitabiriwa kwamba vifo vinavyotokana na maradhi yasiyosambaa vitaongezeka kwa asilimia 55 kufikia 2030.

Maradhi yasiyosambaa ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hasa humu nchini ni kama vile shinikizo la damu, maradhi ya moyo, kiharusi, kansa, kisukari, maradhi ya kiakili, ugonjwa wa pumu na maradhi ya selimundu miongoni mwa mengine.

Kulingana na wachanguzi wa masuala ya kiafya, mbali na athari kwa afya, maradhi haya pia yamekuwa donda sugu kwa uchumi wa familia, jamii na nchi kutokana na gharama ghali ya matibabu, huku yakikadiriwa kupunguza kipato cha familia za hapa nchini kwa asilimia 28.6.

Lakini licha ya mzigo huu, wachanganuzi wa masuala ya kiafya wanasema kwamba bado serikali imeendelea kulaza damu katika vita dhidi ya janga hili.

Kwa mfano, kwenye bajeti ya kitaifa ya mwaka wa kifedha wa (FY 2020/21), katika jumla ya fedha zilizoelekezwa kwenye bajeti ya afya Sh111.7 bilioni, ni asilimia 0.44 Sh 500 milioni pekee iliyotengewa kuzuia na kudhibiti NCDs. Isitoshe, kaunti nyingi bado hazijaunda mipango kamili ya kuelekeza rasilimali upande huu wa afya.

Ndiposa majuma mawili yaliyopita muungano wa wahudumu na wagonjwa wanaougua maradhi yasiyosambaa waliungana kutoa matakwa yao kwa Wizara ya Afya kuhusu jitihada za kuzuia na kudhibiti maradhi haya.

Matakwa yao yalihusisha serikali kutilia mkazo jinsi ya kuzuia, kudhibiti na kutibu magonjwa haya katika mipango yake ijayo, serikali ya kitaifa kutekeleza sera zifaazo kuambatana na mifumo ya kimataifa, juhudi zaidi kuchukuliwa kukabiliana na tatizo la upungufu wa dawa na bidhaa za matibabu ya NCDs nchini, na kutekelezwa vilivyo kwa mpango wa afya kwa wote UHC.

Mwaka 2021, Wizara ya Afya ilikadiria gharama ya kuzuia NCDs kuwa Sh377 bilioni. Bila shaka kiwango hiki cha pesa ni kikubwa na mzigo mkuu kwa sekta ya afya ambayo tayari inaugua, suala linalochochea swali je, pesa hizi zitatoka wapi?

Kulingana na Bw John Gikonyo, mwenyekiti wa chama cha watu wanaougua maradhi yasiyosambaa, mbali na kupata ufadhili kutoka kwa washirika wa maendelo, serikali inaweza kupata pesa za kufadhili udhibiti na tiba ya maradhi haya kupitia vyanzo mbali mbali.

“Hii ni pamoja na ushuru kwa bidhaa za tumbaku, vinywaji vya soda na juisi, vyakula vya haraka na apu za kuvinunua. Hii ni kwa sababu hivi vyote vinachangia maradhi ya NCDs, kumaanisha kwamba sharti tupate kitu kutoka kwao.”

Endapo hatua yoyote haitachukuliwa kukabiliana na maradhi haya, wataalamu wa kiafya wanaonya kwamba huenda mambo yakawa mabaya hata zaidi katika siku za usoni.

Kulingana na Dkt Catherine Karekezi, Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa mashirika yanayohusiana na maradhi yasiyosambaa nchini NCDAK, anasema kwamba japo kukabiliana na maradhi haya ni ghali, gharama ya kufumbia janga hili macho ni ghali hata zaidi.

Kulingana na WHO, maradhi haya hufyonza uchumi wa nchi, kuchochea umaskini na kuhatarisha zaidi huduma ya afya. Kwa mfano, magonjwa haya yanakadiriwa kugharimu mataifa kati ya asilimia 3.5 na 5.9 ya jumla ya mapato yao.

Maradhi haya aidha yanakisiwa kugharimu mataifa zaidi ya Sh200 trilioni kila mwaka. Kati ya mwaka wa 2011 na 2025, mataifa yanayostawi pekee yanatarajiwa kupoteza zaidi ya Sh700 trilioni — ambayo ni sawa na jumla ya mapato ya kitaifa ya nchi za Ufaransa, Uhispania na Ujerumani.

Kulingana na WHO suluhu hapa ni kwa mataifa na hasa yanayostawi kama Kenya, kuwekeza katika kuzuia maradhi haya.

Kulingana na WHO, kwa kuwekeza Sh153 kwa kila mtu kwa mwaka, mbali na kuzuia maradhi haya, mataifa ya mapato ya chini na wastani yaweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya milioni nane, na kuzalisha zaidi ya Sh42 trilioni kufikia mwaka wa 2030.

Ndiposa sasa serikali kadhaa za Afrika zimeanza kutilia mkazo suala hili.

Majuma kadhaa yaliyopita mawaziri wa afya kutoka mataifa tofauti barani walikusanyika katika Makala ya 72 ya Kamati ya WHO kuhusu Afrika, jijini Lomé, Togo, na kuidhinisha mkakati mpya wa kurahisisha ufikiaji na utambuzi na matibabu ya maradhi haya.

Mkakati huu kwa jina PEN-PLUS, A Regional Strategy to Address Severe Noncommunicable Diseases at First-Level Referral Health Facilities unahimili kuimarisha uwezo wa hospitali za wilaya na za rufaa kutambua na kudhibiti magonjwa haya mapema ili kupunguza vifo.

Miongoni mwa mambo mengine, mkakati huo unahusisha mpango wa afya kwa wote na kutumia mtazamo wa kijamii katika uhamasishaji, kupima, utambuzi wa mapema na matibabu ya maradhi haya.

Hapa nchini, mwaka jana Wizara ya Afya ilizindua mkakati wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti maradhi yasiyosmbaa (National Strategic Plan for the Prevention and Control of Non-Communicable Diseases) 2021/22-2025/26.

Dkt Ephantus Maree, Mkuu wa Idara ya maradhi yasiyosambaa katika Wizara ya Afya anasema kwamba serikali tayari imefanya mengi.

“Kwa mfano, kama wizara, tumejaribu kuhusisha watu wanaoishi na maradhi haya hata katika viwango vya sera. Pia, serikali imefanya mengi kuhakikisha ushuru unatozwa kwa bidhaa za tumbaku,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Polisi watibua maandamano ya Azimio IEBC

MUME KIGONGO: Mazoezi ya jioni kwa waume bora kuliko asubuhi

T L