• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Presha yazidi tiketi ya urais ya Azimio iwe Raila-Karua

Presha yazidi tiketi ya urais ya Azimio iwe Raila-Karua

NA KALUME KAZUNGU

SHINIKIZO zimezidi kutolewa kwa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kumteua kiongozi wa NARC Kenya, Bi Martha Karua, kuwa mgombea mwenza wa Bw Raila Odinga katika kura ya urais.

Wanasiasa wa kike watakaowania nyadhifa mbalimbali Lamu kupitia vyama tanzu vya muungano huo, wamesisitiza kuwa Bi Karua ndiye anayefaa zaidi kama naibu wa Bw Odinga endapo Azimio itaunda serikali ijayo.

Mbunge Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo (Jubilee), alisema wanawake wa Kenya watapata matumaini kwamba uongozi wa jinsia ya kike unatambuliwa na kuheshimiwa vilivyo nchini, endapo Bi Karua atateuliwa kwa nafasi hiyo.

Mwaniaji huyo wa ubunge wa Lamu Mashariki katika kura ya Agosti 9 alisema kuwa, Bi Karua akiwa Naibu Rais ataleta uongozi bora unaowajali maskini na wasiojiweza katika jamii.

“Uongozi wa jinsia ya kike mara nyingi huwajali wanyonge,” akaeleza Bi Obbo.

Mwaniaji wa ubunge wa Lamu Magharibi, Bi Maryimmaculate Nyagah (Narc Kenya), alisema kinara wake ni mmoja wa wanasiasa wachache mno ambao wanathamini uongozi bora usiojihusisha na ufisadi.

Wengine waliompigia debe Bi Karua ni Loyce Dama Luwali (Narc Kenya), Nana Mote (Jubilee) na Esha Nizar (ODM) ambao wote wanawania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Kike Lamu.

Kauli yao inajiri wakati kamati maalum ya kupiga msasa watakaofaa kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga, inatarajiwa kuanza rasmi shughuli leo Jumatano.

Mbali na Bi Karua, wengine wanaopendekezwa kutwaa wadhifa huo ni Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Mbunge wa zamani wa Gatanga, Peter Kenneth, Waziri wa Kilimo, Peter Munya, Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Kaunti ya Murang’a, Sabina Chege, Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, na Mbunge wa Kieni, Kanini Kega.

  • Tags

You can share this post!

Ni Nassir vs Sonko kivumbi Mombasa kukabana koo –...

Korti yaokoa mzazi kumpeleka mtoto katika shule ghali

T L