• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Ni Nassir vs Sonko kivumbi Mombasa kukabana koo – Ripoti

Ni Nassir vs Sonko kivumbi Mombasa kukabana koo – Ripoti

NA WINNIE ATIENO

USHINDANI wa ugavana katika Kaunti ya Mombasa utakuwa mkali kati ya vyama viwili tanzu vya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, kwa mujibu wa kura ya maoni.

Ripoti ya utafiti iliyotolewa Jumanne ilionyesha kuwa, Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir wa Chama cha ODM, na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Bw Mike Sonko (Wiper) watakabana koo katika kinyang’anyiro hicho.

Ripoti hiyo ya shirika la utafiti la TIFA inasema kuwa, endapo uchaguzi ungelifanywa leo, Bw Nassir angeibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 40 ya kura akifuatwa na Bw Sonko (asilimia 28).

Aliyekuwa Seneta wa Mombasa Bw Hassan Omar yupo nafasi ya tatu kwa asilimia tisa, huku Naibu Gavana wa Mombasa Dkt William Kingi akiwa na asilimia moja.

Wawili hao watawania ugavana kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Pamoja African Alliance (PAA), mtawalia.

Asilimia 22 ya wapigakura hawajaamua watampigia nani kura ya kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho.

Hata hivyo, Bw Nassir alikosoa ripoti hiyo akisema utafiti haukufanywa ipasavyo.

“Ninavyojua ni kwamba tutapata kura nyingi zaidi ya ilivyotabiriwa. Waende wakafanye utafiti wa kina,” akasema katika mahojiano na Taifa Leo.

Imebainika Azimio inayoongozwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, bado ina ufuasi mkubwa Mombasa kwa asilimia 41 Mombasa, huku Kenya Kwanza ya Naibu Rais William Ruto ikiwa na asilimia 27.

Aidha, wapigakura asilimia 32 hawajaamua upande wanaoshabikia.

Ripoti inaonyesha idadi kubwa ya wapigakura Mombasa hawajaamua ni nani watampigia kura kuwa seneta au mbunge mwakilishi wa kike.

Katika useneta, asilimia 76 ya wapigakura hawajaamua wanayemtaka huku asilimia 78 wakisema hawatamchagua yeyote miongoni mwa wanaoshindania nafasi ya mbunge wa kike.

Seneta Mohammed Faki wa ODM anaongoza kwa asilimia 14 akifuatiwa na Hamisi Mwaguya wa UDA kwa asilimia saba.

Abdulsalaam Kassim (Wiper) na Hazel Katana (Jubilee) wana asilimia moja.

Kwa ubunge wa kike, Bi Asha Mohammed anayetetea kiti hicho anaongoza kwa asilimia nane kish Bi Zamzam Mohammed kwa asilimia saba.

ODM ilimkabidhi tikiti Bi Zamzam lakini Bi Asha akawasilisha malalamishi ambayo uamuzi unasubiriwa.

Amina Abdalla (Jubilee) ana asilimia tatu, wakili Fatma Barayan (UDA) asilimia mbili, na mwanarakati Hamisa Zaja asilimia moja.

“Asilimia 76 ni kubwa sana, hii ni dhahiri ni sharti tujitahidi kueleza wapigakura umuhimu wa maseneta. Wapigakura wengi wameweka mkazo viti vya gavana na urais,” akasema Bw Mwaguya.

Utafiti huo ulifanywa pia Kaunti za Nairobi ambapo ilipatikana Johnson Sakaja angelishinda ugavana kwa asilimia 23 akifuatwa na Polycarp Igathe (asilimia 15).

Katika Kaunti ya Makueni, ilibainika Mutula Kilonzo Jnr angelishinda ugavana kwa asilimia 50, na kumwacha mbali Patrick Musimba ambaye angelizoa asilimia tano pekee katika nafasi ya pili.

Bw Odinga ndiye maarufu zaidi katika kaunti zote tatu, sawa na muungano wake wa Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool yadengua Villarreal ya Uhispania na kutinga...

Presha yazidi tiketi ya urais ya Azimio iwe Raila-Karua

T L