• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:16 PM
Raila ahudhuria kikao cha kukaanga Cherera na wenzake kisha alaani pendekezo la kuwatimua

Raila ahudhuria kikao cha kukaanga Cherera na wenzake kisha alaani pendekezo la kuwatimua

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Martha Karua ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao cha kusikilizwa kwa mapendekezo ya kuondolewa afisini kwa makamishna wanne waliopinga matokeo ya urais mnamo Agosti 15, 2022.

Kikao hicho cha Kamati ya Bunge Kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) katika ukumbi wa County, Nairobi, kiliashiria mwanzo wa mchakato wa kuondolewa afisini kwa Naibu Mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera na makamishna Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi.

Makamishna hao waliwakilishwa mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tharaka George Murugara, na mawakili Apollo Mboya (Cherera), Jotham Orwa (Nyang’aya), Donald Kipkorir (Masit), Danstan Omari (Cherera), Sam Nyaberi (Cherera) na Ndoro Gichamba (Wanderi).

Mapendekezo ya kuondolewa afisini kwa makamishna hao yaliwasilishwa na Chama cha Republican Liberty, Kasisi Denis Ndwiga Nthumbi, Steve Jerry Owuor na Geoffrey Lang’at.

Wamewashtaki makamishna hao wanne kwa kukiuka katiba, kutumia vibaya mamlaka ya afisi zao, kudhihirisha utovu wa ufahamu wa majukumu yao miongoni mwa makosa mengine.

Akiongea baadaye Bw Odinga alisema mchakato wa kuondolewa afisini kwa Bi Cherera na wenzake, unaoongozwa na bunge, haujazingatia haki na umechochewa kisiasa.

“Huku Wakenya wakizongwa na matatizo mengi, nguvu hazifai kuelekezwa katika kuwaondoa afisini makamishna wanne waliotofautiana na mwenyekiti wao. Shughuli hii inayoendelezwa na wabunge haina maana yoyote na inaongozwa na haja ya kulipiza kisasi. Hatua hii inafaa kusitishwa. Haitaisha vizuri,” Bw Odinga akasema.

Alitisha kuwa ikiwa mchakato huo, wa kuondoa afisini makamishna hao wanne, utaendelea hiyo itakuwa mwanzo wa maandamano ya Wakenya dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.

“Na tutaongoza na kushiriki maandamano hayo waziwazi,” Bw Odinga akasema kwenye kikao na wanahabari katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga, mtaa wa Upper Hill, Nairobi.

Hata hivyo, wabunge wa mrengo wa Azimio ambao ni wanachama wa JLAC  waliwaacha makamishna hao wanne “wakisulubishwa” na wenzao wa Kenya Kwanza (KKA), kwa kuondoka kutoka kikao hicho cha kamati ya JLAC.

Hii ni baada ya wao wabunge hao wakiongozwa na kiranja wa wachache Junet Mohamed kuondoka kutoka kikao cha Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba (JLAC) iliyokuwa ikisikiliza pendekezo la kutimuliwa kwa Bi Cherera na Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi.

Hatua hiyo inawaweka Cherera, Masit na Bw Nyang’aya na Wanderi katika hatari ya kung’olewa mamlakani kwa sababu kamati hiyo inahitaji wabunge watatu pekee kuidhinisha hatua hiyo.

Bw Mohamed na wenzake pamoja na mawakili wa makamishna hao, waliondoka wakidai JLAC haikuwa na mamlaka ya kusikiliza suala hilo.

Walishikilia kuwa suala hilo linapasa kushughulikiwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), IEBC yenyewe, au Kamati ya Bunge kuhusu Mamlaka na Hadhi ya Bunge.

Wabunge walioandamana na Junet ni pamoja na T. J Kajwang (Ruaraka), Stephen Mogaka (Mugirango Magharibi), Aden Daudi (Wajiri Magharibi), Farah Maalim (Dadaab) na Adipo Okuome (Karachuonyo).

“Mwenyekiti, tusijihusishe na sarakasi hizi. Makamishna hawa ni Wakenya wanaohudumia nchi hii. Hatuwezi kushiriki katika kikao cha kangaroo ambapo sheria, na haki haiheshimiwi. Hii ni dharau kwa Katiba. Bure kabisa!” Bw Mohamed akafoka huku akiondoka kutoka ukumbi wa County ambamo JLAC ilikuwa ikisikiliza pendekezo kutoka chama cha Republican Liberty.

  • Tags

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Hadhari iwepo katika kubuni maneno ya lugha...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay na Korea Kusini watoshana...

T L