• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Raila alijikwaa kutegemea pakubwa Uhuru – Wadadisi

Raila alijikwaa kutegemea pakubwa Uhuru – Wadadisi

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga aliyeshindwa kwa mara ya tano katika uchaguzi wa urais wa Agosti 09, 2022, alikosea kwa kumwamini zaidi Rais Uhuru Kenyatta na kuwatema washirika wake wa kisiasa wa miaka mingi.

Ukuruba wake na Rais Kenyatta ulimfanya atofautiane na washirika wake wa kisiasa ambao walijiunga na mpinzani wake mkuu Rais mteule William Ruto.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba, Bw Odinga alifanya makosa kumwamini Rais Kenyatta na serikali yake kupiga jeki nafasi yake ya kushinda urais.

“Bw Odinga alitegemea Rais Kenyatta kupenya eneo la Mlima Kenya huku umaarufu wa kiongozi wa nchi katika eneo hilo ukiwa umefifia. Hii haikumsaidia hata baada ya kumteua Bi Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake,” alisema mchanganuzi wa siasa Thomas Maosa.

Anasema kwa kufuata ushauri wa Rais Kenyatta, Bw Odinga aliwatema washirika wake wa kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2017 wakiwemo washauri wake wa miaka mingi na kutegemea serikali katika kampeni zake.

“Bw Odinga alipoanza ushirika wake na Rais Kenyatta kufuatia handisheki yao 2018, aliwatenga washirika wake kama kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na Moses Wetang’ula ambao walikuwa wamemuunga mkono tangu 2013. Pia aliwaweka kando wandani wake kama James Orengo na kukumbatia Junet Mohamed,” asema Bw Maosa.

Japo Bw Kalonzo alijiunga naye katika Azimio, alikataa kumteua kuwa mgombea mwenza wake.Mchanganuzi mwingine wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema ukuruba wa Bw Odinga na Rais Kenyatta ulimpofusha waziri mkuu huyo wa zamani akapoteza umaarufu katika ngome za wanasiasa aliowatenga.

“Ni wazi kuwa kutengana na vigogo wa kisiasa eneo la magharibi kama vile Moses Wetangula na Musalia Mudavadi kulikuwa pigo kwa Bw Odinga. Kulipunguza umaarufu wake katika kaunti za Vihiga na Bungoma,” akasema.

Wachanganuzi wanakubaliana kwamba, kwa kutegemea Rais Kenyatta na kuahidi kuendeleza ajenda zake zilizomkosesha umaarufu na serikali kumfanyia kampeni, Bw Odinga alichelewa kuanza kampeni zake tofauti na Dkt William Ruto aliyeanza mapema.

“Uhuru alipokuwa akisema wakati wa siasa ulikuwa bado, Dkt Ruto alikuwa akijipigia debe jambo ambalo lilimwezesha kupata umaarufu maeneo mengi nchini,” asema Bw Maosa.

Kupitia juhudi za Rais Kenyatta, Bw Odinga aliunda muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ulioleta pamoja vyama 26 vya kisiasa nchini.

Hata hivyo, vyama hivyo vilijiondoa vikidai muungano huo haukuwa na uwazi. Miongoni mwa vyama hivyo ni Pan African Alliance (PAA) cha aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi na Maendeleo Chap Chap cha Dkt Alfred Mutua ambaye alikuwa gavana wa Machakos.

Bw Gichuki anasema kwamba, baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Azimio utasambaratika.

“Muungano huo uliletwa pamoja na Rais Kenyatta ambaye alilenga kuutumia kuwa na ushawishi iwapo Bw Odinga angeshinda urais na jinsi hali ilivyo sasa hakuna matumaini kwamba utadumu,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Makamishna 4 waasi waunga Chebukati

Mshukiwa wa ugaidi aliyetoweka arejea akiwa mzima

T L