• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:50 AM
Raila anyenyekea wazito Mlima Kenya

Raila anyenyekea wazito Mlima Kenya

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, sasa ameanza kuwinda mabwanyenye wenye ushawishi Mlima Kenya katika juhudi zake za kujipenyeza kisiasa katika eneo hilo ambalo limekuwa kizingiti kwa azma yake ya kuingia Ikulu.

Katika juhudi za kufanikisha azima yake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, Bw Odinga anaonekana kuwalenga wafanyabiashara wakubwa wa eneo hilo wampigie debe.

Bw Odinga amefanya mikutano ya mashauriano na wanachama wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF), katika kile kinachoonekana kama sehemu ya mbinu yake mpya ya kupata uungwaji mkono kutoka eneo hilo lenye zaidi ya wapiga ikura milioni tano.

Mnamo Alhamisi, alikutana na viongozi na wasomi kutoka kaunti ya Meru kupitia juhudi za mabwenyenye hao.

Katika mikutano kadhaa ambayo amefanya na wafanyabiashara mashuhuri wa eneo hilo, waziri mkuu huyo wa zamani amekuwa akifafanua jinsi serikali yake italinda maslahi yao na ya wakazi wa eneo pana la Mlima Kenya.

Mnamo Agosti 13 Bw Odinga alikutana na wafanyabiashara na wanasiasa kutoka eneo hilo nyumbani kwa mfanyabiashara tajiri Nginyo Kariuki eneo la Limuru. Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ambapo siasa zilishamiri ni Afisa Mkuu wa Kitengo cha Biashara katika Benki ya Equity, Polycarp Igathe na aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth.

Katika mkutano huo, Bw Odinga alifafanua jinsi sera yake ya uchumi itafaidi wakazi wa Mlima Kenya.

Bw Odinga pia amezuru kaunti ya Murang’a mara mbili mwezi huo ambapo alipata mapokezi kutoka kwa miongoni mwa wengine, mfanyabiashara mashuhuri S. K Macharia.

Mnamo Alhmisi, kiongozi huyo wa ODM alirusha chambo tena katika eneo la Mlima Kenya Magharibi ambapo alifanya mkutano na wafanyabiashara na wataalamu kutoka jamii ya Ameru, katika Safari Park Hotel, Nairobi.

Mkutano huo ulipangwa na MKF, ishara kwamba wanachama wa wakfu huo wenye uhusiano wa karibu na Rais Uhuru Kenyatta, wanaunga mkono azma ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu 2022.

Wakfu huo, ambao wanachama wake pia ni wenye ushawishi mkubwa serikalini, ulipiga jeki kifedha, kampeni za Rais Kenyatta kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 .

Katika mkutano huo wa kupanga mikakati ya kisiasa, ujumbe kutoka jamii ya Ameru, uliongozwa na Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Naibu Kiranja katika Bunge la Kitaifa Maoka Maore (Mbunge wa Igembe North), Jaji Mstaafu na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa iliyokuwa Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini (KACC) Aron Ringera na aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Usalama Mutea Iringo.

Wengine walikuwa Mwenyekiti wa mradi wa Lapsset Titus Ibui, aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Elimu, Kilemi Mwiria na kaimu Gavana wa Nairobi, Anne Kananu.

Viongozi hao waliapa kuvumisha azma ya urais ya Bw Odinga katika eneo hilo huku wakiyeyusha dhana kwamba kiongozi huyo wa ODM hawezi kukumbatiwa na wakazi wa Mlima Kenya kwa ujumla.

“Maneno machafu yalitumika kumsawiri Bw Odinga kama mtu hatari na asiyefaa kuwa rais miaka ya nyuma aliposhindana na Rais mstaafu Mwai Kibaki na rais wa sasa Uhuru Kenyatta. Lakini wakati huu ambapo wawili hao hawagombei tena, hatuna budi kumuunga mkono kwa kusimama nasi tangu 2002,” Bw Murungi alinukuliwa akisema kwenye mkutano huo.

Kwa upande wake, Bw Odinga aliahidi kupiga jeki uzalishaji wa miraa, majani chai, kahawa, ufugaji ng’ombe wa maziwa miongoni mwa sekta zingine ambazo ni tegemeo la wakazi wa Mlima Kenya.

Mkutano huo umejiri siku chache baada ya wabunge kutoka eneo hilo wandani wa Rais Uhuru Kenyatta kuungama peupe kuwa ni vigumu kushawishi wakazi wa eneo hilo kumuunga mkono Bw Odinga.

You can share this post!

Kamishna ataka serikali impe ndege ya kusaka wanafunzi

TSC yaadhibu walimu wanaotoza karo zaidi