• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Raila aongeza kasi ya presha kwa Ruto

Raila aongeza kasi ya presha kwa Ruto

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga, jana alitangaza hatua za kuongeza kasi na presha ya mapambano ya muungano huo wa upinzani dhidi ya serikali ya Rais William Ruto iwapo haitabadilisha sera zake anazosisitiza zinakandamiza raia.

Katika tamko kali zaidi tangu alipoanza mikutano ya hadhara anayoita Mabaraza ya Raia, Bw Odinga alisema Azimio iko tayari kuongoza Wakenya kuandamana ili kuokoa maisha yao kutokana na mzigo mzito wa gharama ya maisha wanaobebeshwa na serikali kupitia sera zake za ushuru.

Bw Odinga alisema iwapo serikali ya Kenya Kwanza, anayosisitiza ni haramu, haitapunguza bei za bidhaa kama unga, stima, mafuta, sukari, maziwa, petroli na diseli, ndani ya siku kumi na nne, Wakenya wataandamana kote nchini “ kurejesha mamlaka yao na kurekebisha hali.”

“Tumekuwa tukizungumzia kuhusu kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu kama unga, stima, deseli na maziwa miongoni mwa zingine kwa muda mrefu. Tumelalamika kuhusu kuongezwa kwa ushuru na hivi majuzi tumezungumzia kuhusu watoto kuacha shule kwa kukosa karo,” Bw Odinga alisema akihutubia mkutano wa maombi ambao Azimio iliandaa katika Jeevanjee, Gardens, Nairobi.

Aidha, aliitaka serikali kurejesha ruzuku za bidhaa za chakula na elimu akisema kuziondoa wakati nchi inakumbwa na kiangazi na njaa ni kutojali Wakenya.

“Hivyo basi,” akasema Bw Odinga, “ni lazima ruzuku hizo zirejeshwe, bei ya bidhaa muhimu na ushuru upunguzwe ndani ya siku 14 zijazo la sivyo tutachukua hatua za kuandamana.”

Rais Ruto aliondoa ruzuku za bei za mafuta na unga baada ya kuingia mamlakani mwaka jana, akisema hazingeweza kudumishwa.

Matamshi ya Bw Odinga yanaweza kufungua sura mpya ya mapambano ambayo Azimio ilianza dhidi ya serikali kufuatia kile ambacho upinzani unataja kama ufichuzi unaoashiria huenda alishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022. Katika mkutano wa kwanza katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi mwezi jana, Bw Odinga alitangaza kuwa Azimio haitambui ushindi wa Rais Ruto, serikali yake na sera zake zote.

Katika mikutano iliyofuatia katika uwanja wa Jacaranda, Kibra, Mavoko, Kisumu na Kisii, kiongozi huyo wa ODM amekuwa akishambulia serikali huku akishauri wafuasi wake kusubiri mwelekeo zaidi kutoka kwake.

SAVA

Kwenye mkutano wa jana Jumatano, alizidisha masharti yake kwa serikali akitaka sava za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kufunguliwa na shirika la kuheshimiwa la kimataifa ndani ya siku 14 ili ukweli ubainike.

Ripoti ambayo Azimio inahusisha na mfichuzi inaonyesha Bw Odinga alishinda urais kwa kura 8.1 milioni dhidi ya 5.7 milioni za Rais Ruto.

Kuhusu mchakato wa kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambao Rais Ruto ameanza, Bw Odinga alizidishwa presha usitishwe hadi pale jopokazi huru la kuteua makamishna litaundwa.

Bw Odinga alisema Azimio haiko tayari kuacha shinikizo zake za kulinda na kuhakikisha haki katika uchaguzi, haki ya kijamii na kiuchumi “hadi itapokitwa kabisa katika mchangawa nchi yetu.”

  • Tags

You can share this post!

Romelu Lukaku abeba Inter Milan dhidi ya FC Porto katika...

Matamshi yenu yapaswa kuambatana na vitendo, Askofu Muheria...

T L