• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
Raila ataka mradi wa Galana Kulalu usimamiwe na serikali za kaunti

Raila ataka mradi wa Galana Kulalu usimamiwe na serikali za kaunti

NA ALEX KALAMA

KINARA wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amependekeza mradi wa kilimo wa Galana Kulalu ukabidhiwe kwa serikali za kaunti ili ziendeleza shughuli hiyo ya kilimo.

Akizungumza katika eneo la Dabaso, kaunti ya Kilifi, Odinga amesema iwapo mradi huo utakabidhiwa serikali za kaunti Kilifi na Tana River basi huenda shida ya njaa ambayo imekuwa ikizikumba kaunti hizo kwa mda mrefu ikapata suluhu ya kudumu.

“Ule mradi wa Galana Kulalu uliletwa hapa kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya watu wa eneo hili kwa upande wa chakula lakini umelala. Sisi kama Azimio tunapendekeza ya kwamba mradi huo uletwe chini ya serikali ya kaunti ya Kilifi na ile ya Tana River wakishauriana pamoja na Bodi ya Kitaifa ya Kilimo cha Unyunyuziaji ili Gavana Gideon Mung’aro asimamie upande huu na Gavana Gadho Godhana asimamie upande ule mwingine ili mradi usaidie watu wa Kilifi na Tana River.

Kiongozi huyo wa Azimio amepuuzilia mbali kauli za baadhi ya viongozi wa mrengo wa Kenya Kwanza ambao wanasema wakati wa siasa umekwisha na hivi sasa ni wakati wa kufanya kazi.

Kinara wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga (wa pili mbele kushoto). PICHA | ALEX KALAMA

“Sasa mimi nimesikia yote ambayo hawa watu wanasema eti wakati wa siasa umekwisha… siasa imekwisha. Siasa gani imekwisha? Kwa sababu uongozi ni siasa ‘governance is political’ huwezi kusema unafanya kazi na umewacha siasa huo ni uongo. Siasa na maendeleo vimeshikana kama mbwa wawili ambao wanalala pamoja,” amesema Bw Odinga.

Mbali na hayo, kiongozi huyo wa upinzani amebainisha kwamba ifikapo tarehe Saba mwezi huu wa Disemba wataandaa mkutano katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi ili kuwauliza Wakenya ikiwa wanakubali makamishina wanne wa IEBC walio tofautiana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati wakati wa kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi kuenda nyumbani au la.

“Hii Kenya sio mali ya Bw (Rais) William Ruto kwa hivyo tunasema hapana. Kenya mpaka iwe nchi ya kidemokrasia. Ndio sababu tunasema tarehe saba ambayo ni Jumatano ijayo tutaenda kule uwanjani Kamukunji na kuuliza Wakenya wote wafike pale, tushauriane ili tuweze kuwaambia ikiwa wanakubali Juliana Cherera na wenzake watatu watolewe kwa ofisi waende nyumbani ama hapana,” amesema Bw Odinga.

You can share this post!

Kiungo Wyvonne Isuza astaafu soka

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 14 | Desemba 4, 2022

T L