• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:36 PM
Raila awashauri wabunge wa Azimio wawe wakiomba idhini yake kabla ya kukutana na Ruto

Raila awashauri wabunge wa Azimio wawe wakiomba idhini yake kabla ya kukutana na Ruto

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amesisitiza kuwa wabunge walioenda Ikulu kukutana na Rais walifaa kupata idhini kutoka kwa uongozi wa chama hicho.

Akiongea wakati wa mkutano wa kundi la wabunge wa muungano wa Azimio (PG) katika mkahawa wa Maanzoni, Machakos, Alhamisi, Bw Odinga alisema wabunge hao wanahadaa kwa kudai kuwa walienda kusaka maendeleo ilhali “ukweli ni kwamba walipelekwa huko na masilahi yao.”

“Chini ya Katiba ya sasa, wabunge hawafai kupiga magoti kwa serikali ili maendeleo yapelekwe katika maeneo yao. Hii ni kwa sababu kila eneo lina haki ya kupata maendeleo,” Bw Odinga akasema.

“Tunashuhudia mtindo mbaya ambapo wabunge wanalazimika kubembeleza serikali ili miradi ya maendeleo itekelezwe katika maeneo yao. Bunge ndio hugawa pesa za maendeleo. Serikali hutengeneza mapendekezo ya bajeti. Bunge huchambua mapendekezo hayo na kuamua namna ya kusambaza pesa hizo za maendeleo,” Bw Odinga akasema.

Bw Odinga alisema kuwa wabunge ambao wanataka kwenda kumwona Rais kuzungumzia masuala ya chama sharti wapate idhini kutoka kwa uongozi wa chama kwanza.

“Ikiwa unataka kwenda kumwona Rais kwa sababu ya mradi fulani wa maendeleo basi nenda tu. Basi ikiwa unataka kwenda kuzungumzia masuala yanayoathiri chama chetu, basi sharti upewe ruhusa na chama. Hawa watu sharti waonekane kama wasaliti katika mkondo wa mapinduzi. Tuko katika mkondo wa suala zito zaidi,” akasisitiza.

Wabunge wa ODM kutoka Luo Nyanza waliokutana na Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua Jumatatu wiki hii walikuwa ni pamoja na; Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki, Huru) Phelix Odiwuor almaarufu, Jalang’o (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo), John Owino (Awendo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Alhamisi, Bw Jalang’o alifurushwa kutoka kwenye mkutano punde tu Bw Odinga alipowasili kwenye ukumbi wa mkutano.

Mbunge huyo aliamua kuenda zake lakini akasisitiza kuwa hawezi kuomba msamaha kwa kukutana na Rais Ruto akishikilia kuwa angali mwanachama wa ODM na muungano wa Azimio.

“Siwezi kuomba msamaha kwa kukutana na Rais. Ningali mwanachama wa ODM na Azimio. Hizi ni siasa,” Bw Jalang’o akawaambia wanahabari kabla ya kuingia kwenye gari lake na kuondoka.

  • Tags

You can share this post!

Wauzaji ngono walalama kudhulumiwa na wateja wao katika...

Wanasiasa walioshindwa uchaguzini bado wavuna nyadhifa...

T L