• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Raila na Ruto wazidi kulisha Wakenya ahadi hewa

Raila na Ruto wazidi kulisha Wakenya ahadi hewa

NA PETER MBURU

WAKENYA wanazidi kulishwa ahadi butu na wagombeaji wakuu wa urais, hasa Raila Odinga na William Ruto kuhusu jinsi maisha yao yataboreshwa baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

Hii ni kutokana na kuwa ahadi hizo ni porojo tu kwani hazijatilia maanani ukweli wa hali ya kiuchumi nchini kwa sasa na unavyotarajiwa kuwa miaka ijayo.

Kulingana na utathmini wa ahadi zao kwa vigezo vya kiuchumi, nyingi ya ahadi za Bw Odinga na Bw Ruto haziwezi kutimika kwa muda wanaosema, huku zingine zikihusu mambo ambayo hata sasa yapo, japo utekelezaji ndio umekuwa tatizo.

Akiwa mjini Thika mnamo Jumamosi iliyopita, Bw Odinga alieleza kuwa endapo atachaguliwa, serikali yake itawafadhili vijana na akina mama kwa mikopo ya riba ya chini, ili kuwainua kiuchumi.

“Tutawapatia hawa vijana wetu kazi za maana. Wale wanaotaka kuanzisha biashara watapata mikopo kutoka kwa serikali na hawatalipa chochote hadi baada ya miaka saba. Vilevile, tumesema hatutaki kuona KRA ikiwasumbua,” Bw Odinga akasema.

Ahadi hiyo ni “Hekaya za Abunawasi” hasa wakati huu ambao serikali imekuwa ikifanya kila juhudi kukusanya ushuru zaidi, ili kutimiza majukumu ya bajeti. Hivyo ikizingatiwa kuwa yeyote anayetarajia kuwa rais sharti atahitaji kuimarisha ukusanyaji ushuru, ahadi hiyo ya Bw Odinga ni danganya toto tu!

Bw Odinga pia anaepuka kusema ukweli kuwa sharti bunge lipitishe sheria ya kuondolea kikundi fulani ushuru.

Kwa upande wake, Dkt Ruto ameahidi kuwa akishinda urais atatenga Sh100 bilioni kubuni nafasi milioni nne za ajira mwaka wake wa kwanza akishinda.

Idadi hiyo ya ajira ambayo Dkt Ruto anaahidi kuleta ndani ya mwaka mmoja ni zaidi ya mara nne ya nafasi zote za kazi ambazo zimebuniwa nchini tangu Jubilee ilipoingia uongozini 2013, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Fedha na Taasisi ya Takwimu Nchini (KNBS).

Hii inaonyesha kuwa uwezekano kuwa ahadi ya Dkt Ruto kubuni nafasi milioni nne za ajira ndani ya mwaka mmoja ni ndoto ya mchana, hasa kwa kuwa hajaonyesha mikakati mahsusi ambayo itaboresha hali ya uchumi na kuuwezesha kuongeza nafasi za ajira.

Vilevile, wagombea hawa wanakosa kuwaambia Wakenya kuwa hata sasa kuna hazina kama Uwezo, Women Enterprise na Biashara ambazo zilianzishwa ili kutoa mikopo sawa na ile wanayowaahidi vijana na akina mama lakini zimeshindwa kuwafaa.

ELIMU YA BURE

Akihutubu mjini Thika, Bw Odinga pia aliahidi jinsi akichaguliwa serikali yake itafadhili elimu bila malipo kutoka shule za chekechea hadi chuo kikuu.

“Kila mtoto ambaye amezaliwa katika taifa letu hata kama wazazi hawana pesa, atapata nafasi sawa kuanzia chekechea, shule ya msingi, ya upili hadi chuo kikuu kulingana na kipawa chake,” akasema.

Bw Odinga alipotoa ahadi hiyo alipuuza ukweli kuwa Serikali imekuwa ikikumbwa na matatizo ya kifedha kuweza kufadhili elimu bila malipo katika shule za msingi na upili. Kwa sasa Serikali inashikilia kuwa elimu hiyo ni ya bure, lakini wazazi bado wanatozwa karo za juu.

Pesa zinazotengewa vyuo vikuu pia zimekuwa zikipungua huku baadhi ya vyuo vikiongeza karo.

“Idara ya serikali ya vyuo vikuu imekumbwa na changamoto zikiwemo ukosefu wa fedha kwa vyuo vikuu vya umma, kwani pesa zote zilizotengwa ziligharamia asilimia 57 tu, badala ya 80 inayohitajika,” Wizara ya Fedha ikasema kwenye bajeti ya 2021/22.

Vilevile, Hazina ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Helb) nayo inazidi kupunguza kiwango cha ukopeshaji huo.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga afika katika uwanja wa Kamukunji kuhutubia raia. PICHA/EVANS HABIL

Hivyo, ahadi ya kusomesha kila mtoto Mkenya bure inamaanisha kuongezwa kwa bajeti ya elimu kwa viwango vikubwa, pesa ambazo serikali haiwezi kupata kwa sasa kutokana na majukumu mengine kama vile madeni.

Bw Ruto na Bw Odinga pia wameahidi kuhakikisha kuwa kila Mkenya atapata matibabu bila malipo kwa kujumuishwa katika bima ya NHIF hata kwa wasio na uwezo wa kulipia.

“Kila Mkenya akiwa mgonjwa, atapata matibabu. Kila Mkenya atakuwa ndani ya bima ya matibabu na yule ambaye hawezi kulipa atalipiwa na serikali,” Bw Odinga amesema.

“Kabla ya mwisho wa mwaka huu, kila Mkenya aliye na miaka 18 kwenda juu atakuwa na bima ya afya ya NHIF na kila mtu atalipa kulingana na mapato yake, na wale wasio na uwezo wa kulipa watalipiwa na serikali. Kila mmoja wetu ataenda hospitalini, kutibiwa bila kuitishwa hata senti,” Dkt Ruto naye ameahidi.

Kinaya ni kuwa wawili hao wanapotamka hayo, Serikali inapanga kupunguza bajeti kwa Wizara ya Afya kwa mujibu wa makadirio ya bajeti kati ya 2020/21 na 2023/24.

Wagombea hawa hawajaeleza ni vipi wanapanga kutekeleza ahadi hiyo ya matibabu nje ya makadirio ya bajeti ambayo huandaliwa kufuatia mashauriano na wataalamu.

You can share this post!

Mauaji ya Wakenya kiholela yazidi miili 19 ikipatikana Mto...

TUSIJE TUKASAHAU: Miradi ya unyunyiziaji maji imekwama

T L