• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Ruto abuni mkakati wa kuangusha Raila Mlima Kenya

Ruto abuni mkakati wa kuangusha Raila Mlima Kenya

Na JAMES MURIMI

WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya, wameamua kuingia vijijini kumpigia debe ili kuimarisha umaarufu wake eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wakizungumza katika hoteli ya Abadare Cottage, Kaunti ya Laikipia baada ya mkutano wa kuweka mikakati ya kampeni na kutetea maslahi ya eneo hilo katika chama cha United Democratic Alliance (UDA), wabunge hao walisema watapeleka mipango ya kiuchumi ya Dkt Ruto mashinani ili kupata maoni ya wakazi.

Viongozi hao walisema kwamba chama cha UDA hakitaungana na vyama vingine kabla ya uchaguzi mkuu ujao mbali kumpigia debe Dkt Ruto na kushirikiana na vingine vilivyo na ajenda kama yake.

‘Yeyote anayezungumza lugha ya watu wa kawaida si adui wetu lakini ni ndugu. Lakini mazungumzo yoyote yatakuwa kupitia UDA,’ alisema Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki. Wabunge hao walikanusha kwamba mkutano huo ulijadili suala la mgombea mwenza wa Dkt Ruto kutoka eneo la Mlima Kenya.

Mwakilishi Mwanamke wa Nyandarua, Faith Gitau alisema baada ya mazungumzo na wataalamu, zaidi ya wabunge 50 waliamua kuunga ajenda ya Dkt Ruto kuhusu eneo lao.

“Tutawasilisha ajenda hiyo kwa wakazi kwenye mikutano katika vijiji, vituo vya kibiashara na masoko miongoni mwa maeneo mengine,” akasema.

Hata hivyo mbinu hii inalenga kukabili juhudi za washirika wa Rais Uhuru Kenya kumpigia debe kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo hilo.

“Tunataka kupata maoni ya watu, idhini na uungwaji mkono,” alisema Bw Gitau. Seneta Kindiki alisema wakazi wameamua kutumia UDA kwa sababu ya mfumo wake wa kuinua uchumi.

“Tunaalika Wakenya kuungana nasi katika safari hii ya kujenga Kenya iliyo na umoja na ustawi,” alisema Profesa Kindiki.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mkutano huo ni Susan Kihika, John Muchiri, Geoffrey King’ang’i, Rigathi Gachagua, Charity Kathambi, Rahab Mukami, John Mutunga, Jayne Kihara, Patrick Munene, Ndindi Nyoro, Benjamin Gathiru, George Kariuki, Michael Muchira na Githua Wamacukuru.

You can share this post!

Waiguru alia kuhangaishwa tena na EACC

Mbinu za Raila kuzima Mudavadi na Ruto Magharibi