• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Mbinu za Raila kuzima Mudavadi na Ruto Magharibi

Mbinu za Raila kuzima Mudavadi na Ruto Magharibi

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, ameweka mikakati ya kulinda ngome yake ya kaunti sita za eneo la Magharibi dhidi ya uvamizi wa Naibu Rais William Ruto na kuzima umaarufu wa kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi.

Bw Odinga amelenga magavana wa kaunti hizo na viongozi wengine wenye ushawishi mashinani ili kuzima wapinzani.Dkt Ruto amekuwa akipenya Magharibi mwa Kenya kwa kutumia washirika wake wakiwemo wabunge kadhaa huku Bw Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula wanaotoka eneo hilo wakipigia debe umoja wa jamii ya Waluhya.

Bw Odinga amevuta magavana wa eneo hilo upande wake, wakiwemo wa vyama vya Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kwa kuwashirikisha katika kampeni yake ya Azimio la Umoja.

Mnamo Ijumaa, Bw Odinga alikutana na Magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, Sospeter Ojaamong (Busia) Wilbur Otichillo (Vihiga), Wycliff Wangamati (Bungoma) na James Ongwae (Kisii) kuwarai kuunga azima yake ya kugombea urais kwa mara ya tano.

“Tulijadili Azimio la Umoja na kugusia masuala ya kisiasa ya hivi punde,” alisema Bw Odinga kupitia Twitter.B

w Wangamati aliyechaguliwa kwa chama cha Ford Kenya amekuwa akimchangamkia Bw Odinga baada ya kutofautiana na Bw Wetang’ula naye Bw Otichillo alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha ANC cha Musalia Mudavadi.Kulingana na Bw Oparanya, mkutano wao na Bw Odinga ulijadili mbinu za kuunganisha eneo la Magharibi nyuma ya Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Tangu uchaguzi mkuu wa 2007, eneo hilo limekuwa likimpigia kura kwa wingi Bw Odinga.Bw Oparanya alisema kwamba watahakikisha kuwa ODM inalinda kura za eneo hilo kutoka Dkt Ruto na Bw Mudavadi ambao pia wametangaza azima ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Tulijadili jinsi ya kushirikiana kuunganisha eneo nyuma ya ODM,” Bw Oparanya alisema.Gavana huyo alisema kuwa kuanzia wiki ijayo, wataongoza shughuli za kuvumisha ODM sio tu eneo hilo bali pia kote nchini.

Chama hicho kimekuwa kikisajili wanachama mashinani katika juhudi za kujiimarisha kabla ya uchaguzi mkuu ujao.Bw Odinga anasisitiza kuwa Azimio la Umoja linalenga kuunganisha Wakenya na kwamba analenga kuunda muungano mkubwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Tunashirikiana na marafiki wetu katika Jubilee. Vyama vingine vingi vitajiunga nasi tunapojitahidi kuunganisha nchi. Tunaweza kutimiza mengi tukiungana na hii ndiyo kauli mbiu yetu,” alisema Bw Odinga.

Baadhi ya washirika wa Dkt Ruto eneo la Magharibi ni mbunge wa Kimilili Didimas Barasa, Benjamin Washiali wa Mumias Mashariki, aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale na aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa.

Bw Odinga pia amekuwa akishirikiana na Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli anayetoka eneo la Magharibi. Bw Atwoli ameapa kwamba atahakikisha Dkt Ruto hatakuwa Rais baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

You can share this post!

Ruto abuni mkakati wa kuangusha Raila Mlima Kenya

Sijajiunga na DP – Muturi