• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:40 PM
Ruto alia Uhuru alimsaliti huku Raila akimtetea

Ruto alia Uhuru alimsaliti huku Raila akimtetea

NA JUSTUS OCHIENG

NAIBU wa Rais William Ruto amemshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa ‘kumsaliti’ na kuvunja ahadi ya kumuunga mkono katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Naibu wa Rais, hata hivyo, alikiri kuwa hakutia saini mkataba wowote na Rais Kenyatta kuhusiana na ahadi hiyo.

Dkt Ruto alisema kuwa hana majuto kwa Rais Kenyatta kumhepa na badala yake kuunga mkono mpinzani wake mkuu Raila Odinga anayewania urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

“Kusema ukweli, hatukutia saini mkataba wowote wa kulazimu Rais Kenyatta kuniunga mkono 2022. Nilimuunga mkono Rais Kenyatta kwa sababu nilihisi kwamba alistahili kupewa fursa ya kuongoza,” akasema Dkt Ruto.

Aliendelea: “Rais aliahidi kwa hiari yake mbele ya Wakenya kuwa angeniunga mkono.”

Alisema kuwa sasa anapambana na mwana wa makamu wa rais wa zamani (Bw Odinga) na mwana wa mkuu wa nchi wa zamani (Rais Kenyatta).

Dkt Ruto alitoa kauli hiyo huku Bw Odinga akisema kuwa Rais Kenyatta hatakuwa na ushawishi katika serikali yake.

Kulingana na Bw Odinga, Rais Kenyatta atakuwa mshauri tu wa serikali ya Azimio, haswa katika masuala ya kimataifa.

Wakizungumza katika mahojiano na runinga ya BBC, viongozi hao wawili waliapa kupambana na ufisadi iwapo watachaguliwa Agosti 9.

Dkt Ruto alidai kuwa siasa ya Kenya imekuwa ikidhibitiwa na watu ambao akina baba wao – wazazi –  walishikilia nyadhifa za juu serikalini miaka iliyopita.

Kwa upande wake, Bw Odinga alisema kuwa Rais Kenyatta hatakuwa na usemi katika serikali yake licha ya kushikilia wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio.

“Anaweza kuwa mshauri wa serikali yangu. Anaweza kusaidia katika baadhi ya mambo serikali inafanya haswa katika rubaa za kimataifa,” akasema Bw Odinga.

“Hatapewa wadhifa au majukumu yoyote katika serikali yangu. Rais mwenyewe amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa anastaafu na kwenda nyumbani,” akaongezea.

Bw Odinga alitetea kauli ya Rais Kenyatta aliyotoa majuzi akisema kuwa haendi popote baada ya kukamilisha muhula wake wa pili Agosti.

“Alimaanisha kwamba baada ya kustaafu hataenda nje ya nchi,” alisema Bw Odinga.

Naibu wa Rais alisisitiza kuwa ana mpango thabiti wa kukabiliana na ufisadi iwapo atachaguliwa kuwa rais Agosti.

“Tuna mpango kabambe wa kupambana na ufisadi. Tutatoa fedha za kutosha kwa idara ya mahakama ili iharakishe kesi zinazohusiana na wizi wa mali ya umma,” akasema.

Lakini Bw Odinga alisema kuwa muungano wa Azimio ndio umejitolea kupambana na zimwi la ufisadi.

“Wakenya wanajua kuwa mimi nimesimama imara dhidi ya ufisadi,” Bw Odinga alisema huku akiongezea kuwa atakabiliana na ufisadi bila woga wala mapendeleo

  • Tags

You can share this post!

Saba wakamatwa kwa madai ya wizi

Pwani ni ngome ya Raila, utafiti wa Infotrak waonyesha

T L