• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Ruto, Raila wasukumiwa handisheki

Ruto, Raila wasukumiwa handisheki

NA WAANDISHI WETU

MIITO ya kumhimza Rais William Ruto kufanya mapatano (handisheki) na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga iliendelea kushika kasi jana huku kiongozi huyo wa Azimio akishikilia kuwa maandamano yataendelea yalivyopangwa.

Lakini Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua jana waliendelea kushikilia msimamo mkali wakisema hawatakubali shinikizo za Bw Odinga na wenzake katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

“Sitaiongoza nchi kwa kuzingatia matakwa na shinikizo ninazopewa na washindani wetu,” akasema alipohudhuria ibada ya shukrani katika uwanja wa Kibugua, Kaunti ya Tharaka Nithi.

Lakini Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na wazee wa jamii ya Waluo wametaka viongozi hawa wawili wapatane wakisema maandamano yataathiri uchumi ambao tayari uko katika hali mbaya.

“Hakuna mtu anayetaka handisheki au nusu-mkate, lakini sharti tuwatambue viongozi wote. Sharti usikilize malalamishi yao. Wakati kama huu ambapo hali ni ngumu zaidi, tangu enzi za Rais Moi maamuzi yamefanywa yenye manufaa makubwa kuliko ya mtu mmoja,”Bw Sakaja akasema.

“Siasa za kuwatenga watu wengine sio siasa ya Kenya Kwanza,” akaongeza.

Kwa upande wao, wazee wa Waluo, ambao ni wanachama wa Baraza la Wazee wa jamii hiyo jana Jumapili walimtaka Bw Odinga kufanya mazungumzo na Rais Ruto ili suluhu ipatikane kuhusu malalamishi aliyowasilisha dhidi ya serikali.

Walisema mazungumzo kati ya wawili hao ndiyo njia ya kipekee ya kusitisha mipango ya Azimio kuvuruga shughuli za serikali. Walisema maandamano kuhusu masuala kama vile kupanda kwa gharama ya maisha hayawezi kutoa suluhu ya kudumu kwa changamoto kama hizo.

“Mahakama ilimthibitisha Ruto kama mshindi katika uchaguzi. Kwa hivyo, hamna kile ambacho upinzani utafanya wakati huu kumwondoa mamlakini. Hivyo basi, litakuwa jambo la busara Raila na Ruto kuzungumza kuhusu changamoto zinazoikabili nchi hii,” Mzee Nyandiko Ongadi, aliyezungumza kwa niaba ya wenzake, aliwaambia wanahabari mjini Homa Bay.

Kulingana na Mzee Ongadi, jamii ya Waluo imesalia nyuma kimaendeleo kwa sababu ya kuwafuata viongozi ambao huendesha siasa za upinzani bila kujali athari zake.

“Ninatoa wito kwa watu wa jamii hii kubadili siasa zao ikiwa wanataka kufaulu katika nyanja zote za maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” akasema.

Wito wa Mzee Ongadi umejiri wakati ambapo Bw Odinga amepanga msururu wa maandamano kote nchini kuishinikiza serikali kutimiza matakwa 15 ya Azimio, ikiwemo kupunguza gharama ya maisha.

Wakati huo huo, wazee, viongozi wa kidini na wa kisiasa kutoka jamii ya Maa wametaka malumbano ya kisiasa kati ya mirengo ya Azimio na Kenya Kwanza yakome. Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Maa, Kelena ole Nchoe, viongozi hao hata hivyo walishikilia kuwa hawatabadili tangazo lao kuwa wataunga mkono serikali ya Dkt Ruto.

“Sisi kama viongozi kutoka kaunti za Narok, Kajiado na Samburu, tumekubali kuwa Ruto ndiye alikuwa chaguo la Mungu kwa Wakenya na tumekubali kufanya kazi naye,” Mzee Nchoe akasema wakati wa ibada ya kutoa shukurani kufuatia uamuzi wa mahakama uliodumisha ushindi wa Gavana Joseph ole Lenku.

Lakini akizungumza jana Mombasa, Bw Odinga alisisitiza kuwa maandamano ya raia yataendelea alivyopanga.

Kiongozi huyo vilevile aliisuta serikali kwa kile alichodai ni njama yake ya kutumia baa la njaa kuwafaidi wafanyabiashara wachache watakaokubaliwa kuagiza vyakula kutoka nje bila kulipia ushuru.

Kulingana na Bw Odinga, serikali ilitoa zabuni kwa wafanyabiashara kuleta nchini vyakula mbalimbali kwa madai kuwa wataondolewa ushuru ilhali bei ya bidhaa hizo ni ya juu kuliko kuzinunua humu nchini.

“Hiyo ndiyo biashara wanayofanya kwa jasho la wananchi. Watatumia mabilioni kuleta bidhaa kutoka nje lakini bei itaenda juu zaidi. Hii ni sababu nyingine tunasema serikali hii lazima iende nyumbani,” akasema akiwa katika mkutano wa hadhara eneobunge la Likoni.

Muungano wa Wasagaji Nafaka (CMA), ulikuwa umethibitisha kuwa hakuna mwanachama wao yeyote ambaye amepewa idhini ya kuagiza vyakula bila ushuru hadi sasa. Hili liliibua maswali kuhusu waliopewa zabuni hiyo.

Awali, muungano wa Azimio ulikuwa umeipa serikali makataa ya siku 14 kutimiza matakwa kama vile kupunguza gharama ya mahitaji muhimu ya umma, kushirikisha vyama vyote vikuu katika mchakato wa kuteua makamishna wapya wa Tume ya Uchaguzi (IEBC), na kufungua mitambo ya kompyuta zilizotumiwa kuhifadhi na kupeperusha matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka uliopita, almaarufu sava.

Baada ya muda huo kukamilika juma lililopita, Bw Odinga alitangaza kutakuwa na maandamano makuu jijini Nairobi Machi 20, kuishinikiza serikali kutekeleza matakwa hayo.

Jana Jumapili alipuuzilia mbali ilani iliyotolewa na Waziri wa Usalama, Prof Kithure Kindiki, dhidi ya wananchi kuvamia sehemu zinazopewa ulinzi maalumu na serikali.

Hii ni ikizingatiwa kuwa, uwezekano wa maandamano kufanywa hadi katika Ikulu uko juu iwapo matamshi ya baadhi ya viongozi wa Upinzani, yatazingatiwa.

“Bw Kindiki hujajua mimi ni nani. Wakati nilikuwa napigania demokrasia ulikuwa bado (mchanga). Huu uhuru ambao tuko nao sasa haukuwepo wakati ule. Unafaa utupigie saluti. Tulikuwa tunapigana na simba wenye meno na makucha. Tuling’oa simba meno na makucha akabaki simba kibogoyo kwa hivyo wewe wacha kututisha,” akasema.

Bw Odinga alikuwa ameandamana na wanasiasa wa ODM kutoka Pwani na maeneo mengine ya nchi, pamoja na vinara wenza wa Azimio akiwemo Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), Bi Martha Karua (Narc-Kenya), miongoni mwa wengine.

Walionya polisi wasikubali amri ya kuvuruga maandamano yatakayofanywa na badala yake waunge mkono nia ya maandamano hayo.

“Wewe ofisa ukiona raia mpigie saluti. Tunakutetea kwa sababu pia wewe uko na shida kama wananchi wengine,” akasema Bi Karua.

  • Tags

You can share this post!

Mzee ‘tajiri’ anaswa kwa kutopeleka wanawe 20 shuleni

Watumishi wa umma huenda wakapoteza marupurupu ikiwa...

T L