• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 1:16 PM
Saburi atupwe jela miaka 10 – Uhuru

Saburi atupwe jela miaka 10 – Uhuru

NA MARY WANGARI

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne amesema kuwa angependa kuona Naibu Gavana wa Kilifi Gideon Saburi akisukumwa jela miaka 10 kwa kuhatarisha maisha ya wakazi wa Pwani alipokataa kujitenga alipotoka Ujerumani.

“Hakuna mtu yeyote aliye juu ya maagizo haya hata awe kiongozi maarufu. Anafaa kuwekwa ndani kwa miaka 10 kwa ukaidi wake ili awe funzo kwa wengine wanaopuuza masharti muhimu ya serikali,” akasema Rais alipohojiwa katika redio ya lugha ya Kikuyu Kameme FM.

Alifafanua kuwa amri ya kusitisha usafiri Nairobi, Kilifi, Kwale na Mombasa haihusu walio na sababu thabiti kama vile wafanyabiashara na waajiriwa wanaofanya kazi katika kaunti nyingine.

“Tunataka kazi na biashara ziendelee. Hatuna mvutano na magavana. Serikali kuu pia ina haja na madaktari na wauguzi ndipo tumetoa pesa hizo. Tutaendelea kufanya kazi na kushirikiana nao,” alisema.

Aliahidi kuwa serikali itaweka mikakati ya kutoa malazi na chakula kwa wanaotoa huduma muhimu ili kuepusha watu kusafiri kutoka eneo moja hadi lingine.

“Msiogope kufanya kazi mliyopatiwa na Mungu nasi kama serikali hatutawaachilia, tutawalinda.”

Aidha, aliwataka mapasta watumie redio na runinga kuwafikia washirika wa makanisa yao.

“Kutokana na hali ilivyo, tunaepuka kukusanyika. Kwa mfano, Askofu Ndingi imetubidi kuandaa ibada ya mazishi itakayohudhuriwa na watu wachache mno kwa sasa. Baada ya ugonjwa huu kudhibitiwa tutaandaa hafla kuu ya kumshukuru Mungu kwa maisha yake,” akasema Bw Kenyatta.

Alieleza kuwa watu wanaogua magonjwa mengine na wangependa kusafiri jijini Nairobi kupata matibabu, basi wanafaa kueleza maafisa wa usalama na wataruhusiwa kwenda.

 

You can share this post!

Vilio nzige hatari wakiharibu mimea

CORONA: Hofu katika kambi ya wanajeshi Lanet

adminleo