• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Sicily Kariuki adinda kumfanyia kampeni gavana Kimemia

Sicily Kariuki adinda kumfanyia kampeni gavana Kimemia

NA SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Waziri wa Maji, Sicily Kariuki ambaye alikuwa anamezea mate wadhifa wa ugavana Nyandarua kwa tikiti ya chama cha Jubilee amesema hatamfanyia kampeni gavana wa sasa Francis Kimemia kuhifadhi kiti chake.

Bi Kariuki alijiuzulu uwaziri mnamo Februari kuwania kiti hicho cha kisiasa.

Hata hivyo, mwezi Aprili alipata pigo baada ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee kusemekana kumpa Kimemia tikiti ya moja kwa moja.

“Ninamshukuru kiongozi wa chama Rais Kenyatta kwa kuonyesha usawa, kura za maoni zinaashiria naongoza kwa alama 10 mbele kule nyanjani. Nina uhakika nitaibuka mshindi katika uchaguzi mkuu, Agosti 9,” gavana Kimemia akasema Aprili 28.

Duru zinaarifu waziri Kariuki alishawishiwa kumwachia Kimemia kupeperusha bendera ya ugavana Nyandarua.

Licha ya maafikiano, Kariuki amesisitiza hatamfanyia kampeni mpinzani wake.

“Kwa kufanya hivyo italeta mgogoro. Nilihiari kumwachia agombee,” akasema kwenye mazungumzo na kituo kimoja cha runinga nchini.

“Hata Mungu anajua nilikuwa na mipango mikuu na ya busara kwa watu wa Nyandarua,” Kariuki akaelezea, akisifia rekodi ya utendakazi wake wakati akiwa serikalini.

Kando na Wizara ya Maji, chini ya serikali tawala ya Jubilee, amewahi kuhudumu kama Waziri wa Afya na Utumishi wa Umma, Vijana na Jinsia.

Licha ya kudai wafuasi wake wanamhimiza awe debeni kama mgombea wa kujitegemea, Bi Kariuki alisema hatachukua mkondo huo.

Badala yake alisema: “Nitarejea nyanjani kuwaeleza mwelekeo.”

Alipuuzilia mbali uvumi kwamba uamuzi kumuachia gavana Kimemia ulitokana na makubaliano katika Azimio chini ya unahodha wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa atapata nafasi ya uongozi endapo waziri mkuu huyo wa zamani atafanikiwa kumrithi Rais Kenyatta.

Jubilee ni miongoni mwa vyama vinavyounda mrengo wa Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Uhalifu: Mishi alaumu wanaume kuzembea

Real Madrid yang’oa Man-City na kufuzu kuvaana na...

T L